Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
(Arab League) amelaani jinai za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni dhidi
ya raia wa Palestina.
Ahmad Abul Ghait amelaani jinai za
utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kulitaka Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake katika kuwalinda
raia wa Palestina mbele ya jinai za utawala wa Israel.
Mahmoud Afifi, msemaji wa Katibu Mkuu wa Arab League pia jana
alitahadharisha kuhusu kuendelea jinai hizo za utawala wa Kizayuni huko
Ghaza na kueleza kuwa hali ya mambo katika eneo hilo inahitajia
uingiliaji wa jamii ya kimataifa. Afifi alisisitiza kuwa wale wote
waliohusika na jinai dhidi ya raia wa Palestina huko Ghaza inapasa
wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Maelfu ya Wapalestina tarehe 30 mwezi
uliopita wa Machi walifanya maandamano ya amani katika maadhimisho ya
mwaka wa 42 wa "Siku ya Ardhi" kuelekea katika mpaka wa Ghaza na ardhi
za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; ambapo waandamanaji hao
walikabiliwa na hujuma na mashambulizi ya utawala wa Israel. Katika siku
hiyo ya maandamano hayo ya amani chini ya anuani ya "Haki ya Kurejea",
Wapalestina 17 waliuliwa shahidi na wengine zaidi ya 1400 walijeruhiwa.
Tangu siku hiyo hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 29 wameshauliwa
shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel na wengine zaidi ya
3000 wamejeruhiwa. Nchi nyingi na vile vile taasisi za kimataifa
zimelaani jinai hizo za Wazayuni.
No comments:
Post a Comment