Wednesday, June 13, 2018

MGOGORO WA KIDIPIOMASIA KATI YA KENYA NA UGANDA WANUKIA TENA

Mgogoro mwingine wa kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda unanukia. Hii ni baada ya makumi ya wahamiaji haramu raia wa Uganda kukamatwa na maafisa wa polisi wa Kenya katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Wambua Katiithi, Kamanda Mkuu wa Polisi katika mji wa Bumula, kaunti ya Busia amesema wahajiri haramu 53 wa Uganda wamekatwa wakiwa hawana vyeti vinavyohitajika vya usafiri, wakiwa njiani kuelekea mjini Nairobi kwa kutumia usafiri wa basi.
Tukio hilo lilifanyika hapo jana, ikiwa ni chini ya masaa 24 baada ya polisi ya Uganda kuwatia mbaroni askari polisi watatu wa Kenya na wavuvi kadhaa kati ya visiwa vya Mageta na Hama katika Ziwa Victoria.
Kenya na Uganda zimekuwa zikivutana kwa miaka kadhaa sasa kuhusu masuala kadha wa kadha na haswa umiliki wa kisiwa cha Migingo, kilichoko katika mpaka wa nchi mbili hizo za Afrika Mashariki.
Kisiwa cha Migingo kinachozozaniwa na Kenya na Uganda
Mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kisiwa cha Migingo katika Ziwa Victoria ni milki ya Kenya.
Mgogoro wa kisiwa cha Migingo ulianza mwaka 2008 baada ya wanajeshi wa Uganda kukivamia na kuwatimua Wakenya ingawa kimekuwa kikitambuliwa kuwa ni milki ya Kenya.
Makubaliano ya awali kati ya Kenya na Uganda kuhusu kisiwa hiki yalifanyika 2016, na kwa sasa maafisa wa usalama kutoka nchi zote mbili wanalinda doria katika kisiwa hicho.

No comments:

Post a Comment