Friday, April 13, 2018

MAGAIDI WA BOKO HARAM WAMEWATEKA WATOTO ZAIDI YA 1,000 TOKEA 2013

Magaidi wa Boko Haram wamewateka watoto zaidi ya 1,000 tokea 2013
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria wamewateka watoto zaidi ya 1,000 tokea mwaka 2013.
Hayo yamedokezwa katika ripoti mpya ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto, UNICEF ambayo imetolewa kwa munasaba wa kutekwa wasichana 276 wa shule katika mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria. Wasichana hao walitekwa na magaidi wa kundi hilo la Kiwahhabi la Boko Haram.
Mkuu wa UNICEF nchini Nigeria Mohamed Malick Fall amesema watoto katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi ambayo yanashtua sana. UNICEF imesajili kesi zaidi ya 1,000 za watoto kutekwa nyara lakini imesema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi. Aidha shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema limemhoji msichana aliyewahi kutekwa na Boko Haram ambaye sasa ana umri wa miaka 17 ambaye amesema alinajisiwa na wapiganaji wa kundi hilo. Anasema alipata mimba baada ya tukio hilo la kusikitisha na sasa anakabiliwa na matatizo mengi katika kambi ya wakimbizi huku akikejeliwa kuwa  yeye ni 'mke wa wapiganaji wa Boko Haram'.
Katika usiku wa Aprili 14 kuamkia 15, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara wasichana 276 ambao wengi wameshaachiliwa lakini 100 bado hawajulikani waliko na kuna wasi wasi kuwa baadhi wameshafariki huku baadhi wakiwa wameamua kubakia huko walikotekwa nyara.
UNICEF inasema tokea uanze uasi wa magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria, hadi sasa waalimu zaidi ya 2,295 wameuawa na shule 1,400 kubomolewa.
Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.
Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.

No comments:

Post a Comment