Spika wa Bunge la Federali la Somalia,
Mohamed Sheikh Osman Jawari, hatimaye amejiuzulu baada ya nchi hiyo ye
Pembe ya Afrika kushuhudia taharuki na mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa
wiki kadhaa.
Dahir Amin Jesow, mmoja wa wabunge ameliambia shirika la habari
la Reuters kuwa, "Asubuhi ya leo tulikuwa tunajiandaa kujadili hoja ya
kumuondoa madarakani Spika, mara ghafla Naibu Spika akaja na barua ya
kujiuzulu Spika huyo na kuisoma mbele yetu. Tumepongeza hatua hiyo ya
kujiuzulu ambayo inakubalika kikatiba, na tunatumai huu ndio mwisho wa
mzozo wa kisiasa nchini."
Wiki iliyopita, Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa
Somalia alisimamisha kikao kingine cha Bunge kilichokusudia kujadili
hoja hiyo ya kumuengua madarakani Spika wa bunge hilo.
Somalia imeshuhudia malumbano makali baina ya Waziri Mkuu wa nchi
hiyo Hassan Ali Khaire pamoja na kundi la wabunge wanaomuunga mkono kwa
upande mmoja, na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa
upande mwingine.
Mgogoro huo ulianza mapema mwezi jana, baada ya wabunge zaidi ya
100 wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja bungeni ya
kutaka kuenguliwa madarakani Spika wa bunge, kwa madai kuwa amekuwa
kizingiti kwenye shughuli za bunge hilo.
Mohamed Osman Jawari, Spika wa Bunge la Somalia anatuhumiwa na
wabunge kuwa anatumia vibaya madaraka yake na kuzuia kufanyiwa
marekebisho katiba ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment