DRC yasusia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kukusanya fedha za kuwasaidia raia wa nchi hiyo
Mkutano maalumu uliotishwa na Umoja wa
Mataifa umeanza leo mjini Geneva Uswisi kwa kuchangisha fedha za
kukabiliana na janga la kibinaadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo huku serikali ya Kinshasa ikiususia mkutano huo.
Mashirika ya misaada yanasema kuwa, zaidi ya watu milioni 5
wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia yya
Congo kwa sababu ya mapigano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Aidha mkutano huo wa wafadhili umeanza leo huku takwimu za Umoja wa
Mataifa zikionesha kwamba, watu milioni 13 wanahitaji msaada huku
thuluthi moja kati yao wakiwa ni wakimbizi wa ndani ambao wanahitaji
msaada wa dharura wa kibinadamu mwaka huu.
Wafadhili hao wa kimataifa wanatafuta kiasi cha dola bilioni 1.7
kuwasaidia watu hao wanaohitaji dawa, chakula na makazi mazuri.
Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesusia
mkutano huo, ikiyashutumu mashirika ya kiraia kwa kutoa takwimu za uongo
na kulichafulia jina taifa hilo.
Uamuzi huo wa serikali ya Kinshasa wa kususia mkutano huo
umekosolewa, huku baadhi ya wakosoaji wakisema kwamba, serikali yya
Kinshasa ingeshiriki tu katika mkutano huo ili kuwashajiisha wafadhili
watoe misaada kwani wanaoumia ni raia.
Hayo yanajiri katika hali ya ambayo, hivi karibuni Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa lilionya kuwa, hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuwa mbaya na imefikia hatua ya kuwa
janga kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, huku mamilioni ya watu
wakikabiliwa na njaa.
No comments:
Post a Comment