Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewafuta kazi zaidi ya mahakimu 250 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya ufisadi.
Waziri wa Sheria Alexis Thambwe
Mwamba amesema kuwa, mahakimu hao wamefutwa kazi kwa sababu za ufisadi
na wengine kutokuwa na elimu ya taaluma hiyo.
Waziri thambwe amebainisha kuwa, hatua
hii imechukuliwa ili kuwazuia watu waliokuwa wakiingia katika idara ya
mahakama wakiwa na lengo la kujipatia fedha badala ya kuwatumikia raia
wa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, idadi
kamili ya mahakimu waliofutwa kazi na serikali ni 256 na kwamba, sababu
kuu ni majaji hao kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, kutokuwa na
elimu ya taaluma hiyo na kundi la tatu limestaafishwa.
Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo Kinshasa kuwachukulia hatua maafisa wa juu wa idara ya
Mahakama. Mwaka 2009, Rais Joseph Kabila aliwafuta kazi majaji 96 baada
ya kubainika kuwa walikuwa wakijihusha na vitendo vya ufisadi.
Hatua hiyo ya kufutwa kazi majaji hao
inakuja kukiwa kumesalia miezi 7 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu katika
nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto kubwa ya usalama.
Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike mwishoni
mwa mwaka jana ulisogezwa mbele na sasa unatarajiwa kufanyika Desemba
23, mwaka huu ili kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye muhula
wake wa uongozi ulimalizika Desemba 20, 2016.
No comments:
Post a Comment