Friday, May 12, 2017

WAKIMBIZI WA SUDAN KUSINI WAMIMINIKA SUDAN KWA MAELFU

Maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaendelea kumiminika nchi jirani ya Sudan wakitafuta mahala salama katika nchi ambayo walijitenga nayo miaka kadhaa iliyopita.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono na asilimia 99 ya raia wake baada ya vita vya miongo kadhaa vya kutaka uhuru. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.
Zaidi ya raia 375,00 wa Sudan Kusini, aslimi 90 wakiwa ni wanawake na watoto, wamekimbia Sudan tokea vita vya ndani vianze katika nchi yao mwaka 2013. Uganda nayo ina wakimbizi 883,000 kutoka Sudan Kusini huku wengine wakikimbilia nchi jirani ya Kenya.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema idadi ya Wasudan Kusini wanaokimbilia Sudan inazidi kuongezeka. UNCHR imesema mwezi uliopita pekee raia 23,000 wa Sudan Kusini waliingia  Sudan na kwa ujumla mwaka huu idadi hiyo ni 108,000. Imetabiriwa kuwa mwezi ujao raia wengine 50,000 wa Sudan Kusini watakimbilia Sudan wakitoroka vita na njaa katika nchi yao.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (left) na kiongozi wa waasi Riek Machar
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

No comments:

Post a Comment