Sunday, May 21, 2017

HIZBULLH: SAFARI YA TRUMP SAUDIA NI YA KIWENDAWAZIMU

Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imeitaja safari ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini Saudi Arabia kama ya kiwendawazimu na ambayo haitakuwa na tija yoyote kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Sayyid Hashem Saifuddin, Rais wa Baraza Kuu la Hizbullah amesema Washington haina uwezo wa kudhuru au kuweka kizingiti kwenye shughuli za harakati hiyo ya muqawama.
Amesema safari ya Trump nchini Saudia ni ithibati kuwa Hizbullah inazidi kupata nguvu kila uchao kiasi cha kuwakosesha usungizi na kuwatia kiwewe maadui wa muqawama.
Amesema: "Malengo ya utawala wa kiwendawazimu wa Washington chini ya Trump hayatafikiwa katika safari hiyo ghairi ya kupata kuangaziwa tu na vyombo vya habari."
Trump na Mfalme Salman wa Saudia wakicheza densi mjini Riyadh
Hii ni katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita, utawala wa Riyadh ulitangaza kumuwekea vikwazo afisa huyo wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon. Itakumbukwa kuwa, mwezi Februari mwaka huu, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah alisema Trump ni mtu mpumbavu.
Hivi karibuni, kikao cha siri cha upangaji njama dhidi ya harakati ya Hizbullah kilifanyika mjini Washington, Marekani na kuhudhuriwa na nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi PGCC.

No comments:

Post a Comment