Monday, May 15, 2017

QALIBAF AJIONDOA UCHAGUZI WA RAIS IRAN, AMUUNGA MKONO RAISI

Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf amejiondoa katika mchuano wa kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika taarifa, Qalibaf amewataka wafuasi wake wamuunge mkono Ibrahim Raisi, mgombea mwingine anayewania urais wa Iran. Amesema katika taarifa hiyo: "Kwa ajili ya kuwepo umoja katika mrengo wa mapinduzi,  nimechukua uamuzi muhimu na wa kimsingi. Kwa ajili ya kulinda malengo matukufu ninatoa wito kwa wafuasi wangu kote Iran kutumia uwezo wao wote kuhakikisha Ibrahim Raisi Sadat anafanikiwa kuunda serikali ya 'Kazi na Heshima' kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. 
Mgombea mwingine ambaye ameripotiwa kujiondoa katika duru hii ya 12 ya uchaguzi wa rais wa Iran ni Mustafa Hashemi Taba ambaye Jumatatu alitoa taarifa na kusema atampa kura yake rais wa sasa Hassan Rouhani. Wagombea wengine wa urais ni  Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu na Es'haq Jahangiri makamu wa kwanza wa serikali ya sasa.
Wagombea sita wa urais Iran katika mdahalo siku ya Ijumaa
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran. 
Kamati ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Wairani zaidi ya milioni 56 wametimiza masharti ya kupiga kura na hivyo wanatazamiwa kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais.
Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika vituo 269 vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi 103 kote duniani.

No comments:

Post a Comment