Tuesday, May 16, 2017

KOREA KASKAZINI: KOMBORA TULILOLIFANYIA MAJARIBIO, LINAWEZA KUBEBA KICHWA CHA NYUKLIA NZITO

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa, kombora la balestiki ililolifanyia majaribio siku ya Jumapili iliyopita, inaweza kubeba kichwa cha nyuklia nzito.
Katika jaribio hilo lilisimamiwa na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini. Picha zilizorushwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo zilimuonyesha kiongozi huyo akifuatilia kwa karibu shughuli za urushaji wa kombora hilo. Katika picha zingine, kiongozi huyo alionekana akiwa na makamanda wa jeshi akipiga makofi kwa kuonyesha mafanikio ya jaribio hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi sasa Pyongyang imewekewa vikwazo mbalimbali na Umoja wa Mataifa kutokana na miradi yake ya silaha za nyuklia. Kufuatia jaribio hilo, Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kuiwekea vikwazo vikali zaidi Korea Kaskazini, baada ya Pyongyang kufyatua kifaa kinachoaminika kuwa kombora hilo la balestiki kuelekea upande wa Japan. Taarifa ya Ikulu ya Marekani ya White House ilisema kuwa, uchokozi mpya wa Korea Kaskazini unafaa kuwa kengele ya hatari kwa nchi zote duniani, na kwamba jamii ya kimataifa inafaa kutekeleza vikwazo vikali zaidi kwa nchi hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Marekani yenyewe imekuwa ikifanya majaribio kadhaa ya silaha za nyuklia, mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa. Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa itaendelea kujiimarisha kwa silaha hizo na makombora ya balestiki ili kujiandaa na vitisho na harakati za kijeshi za Marekani na washirika wake katika eneo la Peninsula ya Korea. Katika hatua nyingine, serikali ya Washington na Seoul, zimefikia makubaliano yenye lengo la kuiwekea mashinikizo Korea Kaskazini kutokana na silaha zake hizo hatari.

No comments:

Post a Comment