Tuesday, May 16, 2017

MADAI YASIYO NA MSINGI KWAMBA IRANI INAPELEKA SILAHA NCHINI YEMEN

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi ameashiria mashambulio ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen yaliyoanza Machi mwaka 2015 na kuendelea hadi sasa na kueleza kwamba Wayemeni wana silaha nyingi sana ambapo bila ya kuzingaia ukweli huo, Saudia ilidhani itaweza kuhatimisha vita hivyo kwa manufaa yake ndani ya kipindi kifupi mno.
Qassemi ameyaeleza hayo katika mahojiano na jarida la Al-Arabiyyul-Jadidah linalochapishwa London, Uingereza. Katika mahojiano hayo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amekanusha uvumi kwamba Iran inaisaidia Yemen kwa silaha na kufafanua kwamba baadhi ya nchi zinaituhumu Iran kuwa inapeleka silaha kimagendo Yemen hali ya kuwa kwa upande mmoja, Tehran haijajiingiza kijeshi wala kifedha katika mgogoro wa nchi hiyo na kwa upande mwengine Wayemeni hawahitaji silaha za Iran.
Bahram Qassemi
Aidha amesisitiza kwamba Saudia inapaswa iache tuhuma na siasa zake za kiadui dhidi ya Iran na kwamba endapo itafanya hivyo Tehran iko tayari kufanya mazungumzo ya pande mbili na Riyadh.
Kutangazwa habari za kutumwa silaha kimagendo nchini Yemen kutokea Iran ni upatu unaopigwa na mashirika na vyombo vya habari vya eneo kila baada ya muda ili kupata kisingizio cha kuyakariri madai kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Hata hivyo madai hayo katu hayajaweza kuthibitishwa; na hata Umoja wa Mataifa pia umekiri kuwa hakuna silaha yoyote iliyotumwa kutoka Iran na kupelekewa makundi yanayopigana nchini Yemen. Hata hivyo tuhuma zinazotolewa dhidi ya Iran zinaweza kuwa na malengo mawili. Lengo la kwanza ni kujenga hisia kuwa Iran ina nafasi hatarishi katika eneo. Kwa kutumia kisingizio hicho, Saudia inataka kuonyesha kuwa vita vamizi ilivyoanzisha dhidi ya Yemen na mauaji ya kinyama inayoendelea kufanya kila siku dhidi ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo ni vita vyenye uhalali wa kisheria. Ilhali ukweli ni kwamba uvamizi wa Saudia tokea mwanzo wake ulikuwa na sura ya kichokozi wala hakuna njia yoyote ya kuutetea na kuuhalalisha uvamizi huo.
Ndege za kivita za Saudia zinazofanya mauaji kila leo ya raia wa Yemen
Madai ya kupelekewa silaha harakati ya Ansarullah ambayo kwa kweli inatetea matakwa ya wananchi wa Yemen na kupambana na wavamizi yanatolewa na nchi kama Saudi Arabia na Uingereza. Nchi kama Uingereza inaipatia Saudia silaha zilizopigwa marufuku izitumie katika vita vya Yemen na kimsingi inapaswa kuwajibika kwa hatua yake hiyo. Lakini lengo la pili la kuzushwa madai ya utumaji silaha Yemen kutokea Iran ni kufifilisha kushindwa na kugonga mwamba njama ya Saudia ya kutaka kuidhibiti Yemen. Licha ya kupindukia muda wa miaka miwili tangu ilipoanzisha mashambulio na hujuma za mtawalia dhidi ya Yemen ambazo zimeteketeza miundombinu ya miji, barabara, madaraja na bandari, mbali na kumwaga damu na kuua maelfu ya watu, Saudi Arabia ingali imeshindwa kuidhibiti nchi hiyo huku yenyewe ikiendelea kupata kipigo kikali kutoka kwa muqawama wa wananchi wa Yemen.
Uharibifu unaofanywa na hujuma za Saudia dhidi ya Yemen
Kwa hivyo suala la Yemen linapaswa kuangaliwa kwa upande mwengine. Ni wazi kuwa katika kadhia hiyo umoja wa ardhi yote ya Yemen umevamiwa waziwazi, na lengo la utawala wa Aal Saud ni kuigawa na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo masikini ya Kiarabu au kuyaunganisha baadhi ya maeneo yake na ardhi ya Saudia. Kitambo nyuma televisheni ya utawala wa Aal Saud ilionyesha ramani ya maeneo yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchini Yemen na kuyaelezea kuwa ni sehemu ya ardhi ya Saudi Arabia. Kwa hivyo kujitoa kimasomaso utawala wa Aal Saud hakuwezi kubadilisha ukweli halisi wa mambo.
Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza (kulia) akiamkiana na Mfalme Salman wa Saudia
Lililo wazi ni kuwa vita vamizi na vya kichokozi vilivyoanzishwa na Saudia dhidi ya Yemen vimezidi kuvuruga amani katika eneo la Mashariki ya Kati. Mashambulio na hujuma za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia vimeshamirisha ugaidi na kuwafanya mamia ya maelfu ya raia kupoteza makazi yao na kuwa wakimbizi. Pamoja na hayo ungangari na kusimama imara wananchi na viongozi wa Yemen katika kukabiliana na ugaidi na uvamizi haujatoa ruhusa kwa wavamizi kuzidi kusonga mbele ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Inapasa kusema kuwa  Iran, ambayo ni nchi yenye nguvu katika eneo hili na yenye kutoa mchango chanya na athirifu haina haja ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyengine. Kama ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeunga mkono utatuzi wa kisiasa katika mgogoro wa Syria inaunga mkono pia njia za kisiasa kama suluhisho pekee la kuutatua mgogoro unaoendelea nchini Yemen.../

No comments:

Post a Comment