Monday, May 15, 2017

RAIS WA MAREKANI NA WAZIRI WA ULINZI WA SAUDIA NI WATU HATARI ZAIDI DUNIANI

Gazeti la The Independent linalochapishwa Uingereza limemuelezea Rais wa Marekani na Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia kuwa ni watu hatari zaidi duniani.
Makala iliyoandikwa kwenye toleo la siku ya Jumamosi la gazeti hilo imeashiria safari itakayofanywa siku chache zijazo na Rais Donald Trump wa Marekani nchini Saudia na kuandika kuwa Trump ameiahidi Saudia msaada mkubwa kwa operesheni za kijeshi za Riyadh nchini Yemen; na hivi sasa kaimu mrithi wa ufalme ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudia Muhammad bin Salman anafanya juu chini kuishawishi Washington iiunge mkono nchi hiyo katika kukabiliana na Iran.
Trump na Muhammad bin Salman katika Ikulu ya White House
Katika makala hiyo ya gazeti la Independent imeelezwa kuwa Marekani na Saudi Arabia zimekubaliana kushadidisha misimamo yao dhidi ya Iran; na uamuzi wa kwanza ziliouchukua ni kuziunga mkono jamii za wachache nchini Iran zijitenge na mfumo wa Iran, ambapo ripoti za awali zilizotolewa zinahusu mipango ya pamoja ya Washington na Riyadh ya kuwaunga mkono Mabaluchi wa kusini mashariki mwa Iran.
Ripoti hiyo kupitia makala ya gazeti la The Independent imetolewa katika hali ambayo mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa Gholam-Ali Khoshrou, yapata siku kumi zilizopita alimwandikia barua ya malalamiko Katibu Mkuu na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo akieleza kwamba matamshi yaliyotolewa na Muhammad bin Salman dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu alipotamka kwamba "lengo la Saudia ni kuvihamishia vita ndani ya mipaka ya Iran" ni utoaji vitisho wa wazi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni ukiukaji wa kipengele cha nne cha kifungu cha pili cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Gholam-Ali Khoshrou, mwakilishi wa kudumu wa Iran, UN
Khoshrou alisisitiza kwamba matamshi ya kihasama na kiadui ya Waziri wa Ulinzi wa Saudia si ya utoaji vitisho tu dhidi ya Iran lakini pia yana maana ya kukiri waziwazi utawala wa Aal Saud kwamba unahusika na vitendo vya kigaidi na machafuko vinavyofanywa ndani ya ardhi ya Iran, ambapo kuuliwa shahidi walinzi tisa wa mpakani wa Iran na genge la wahalifu wanaoungwa mkono na kusaidiwa kifedha na Saudia ni mfano wa karibuni kabisa wa suala hilo.
Hoja kwamba siasa za Saudia ni hatari ilishathibitishwa tokea hapo kabla. Kwa hatua zake mbalimbali, Saudi Arabia ilisababisha kuundwa makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na Taliban katika muongo wa 1990 na kuanzia mwaka 2003 ikaunga mkono vitendo vya kigaidi na vya kuvuruga utulivu na uthabiti ndani ya Iraq na kupelekea kuundwa Daesh, Jabhatu-Nusra na makundi mengine ya kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo pamoja na Syria.
Magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh, zao la siasa mbovu za Saudia
Kutokana na mtazamo wa fikra mbovu na potofu ilionao serikali mpya ya Marekani, hivi sasa hatua hizo haribifu za Saudia zimegeuka kuwa fursa kwa utawala wa Aal Saud ya kujionyesha na kuhalalisha sera zake za hujuma na uvamizi dhidi ya nchi za eneo.
Serikali ya Marekani, hasa baada ya kuingia madarakani Donald Trump, imechukua maamuzi yasiyo ya kiutu na kukanyaga usuli na misingi ya hisia za ubinadamu na Hati ya sheria za kimataifa. Mfano hai wa maamuzi hayo ni kuziuzia silaha zilizopigwa marufuku tawala zinazosifika kwa mauaji ya watoto kama Saudia na Israel.
Ushirikiano huo hatari  sasa unaonekana kuingia kwenye awamu mpya kwa safari inayokaribia kufanywa na Trump nchini Saudi Arabia. Athari za mshikamano huo uliopo baina ya Riyadh na Washington zimezidi kudhihirika kwa hatua ya Marekani ya kubariki mauzo ya silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa Saudia na kuwepo ukuruba mkubwa zaidi wa uhusiano kati ya Aal Saud na utawala wa Kizayuni wa Israel, sambamba na kushadidi mbinyo na mashinikizo dhidi ya muqawama wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati. Mwenendo huu umezifanya duru nyingi za kisiasa na za wachambuzi wa masuala ya eneo kufuatilia kwa karibu malengo ya safari inayokaribia kufanywa na Trump huku zikiwa na wasiwasi mkubwa wa maamuzi hatari yanayoweza kuchukuliwa na Marekani na Saudia. Sababu ni kwamba siasa za Washington na Riyadh hazina muelekeo wowote wa kuleta amani na usalama katika eneo hili.../

No comments:

Post a Comment