Sunday, May 28, 2017

47 WAUAWA KATIKA MAPIGANO KATI YA MAKUNDI HASIMU LIBYA

Kwa akali watu 47 wameuawa katika mapigano yanayoendelea katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, kati ya wapiganaji wa makundi mawii hasimu ya kisiasa.
Wizara ya Afya ya Libya imesema mbali na mauaji hayo, watu wengine zaidi ya 180 wamejeruhiwa, huku idadi ya raia miongoni mwa wahanga hao ikikosa kujulikana.
Mapigano hayo yalianza Ijumaa iliyopita, na kushtadi hapo jana hususan katika wilaya za Abu Salim, Salahedeen, na Qasr Bin Ghashthen.
Wapiganaji wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa hata hivyo imesema imepoteza wapiganaji 52 katika mapigano ya jana Jumamosi.
Martin Kobler, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amelaani vikali mauaji hayo na kuzitaka pande zote kukomesha uhasama, kulinda raia na kushirikiana kufikia utangamano wa kitaifa.
Mbali na mapigano ya pande mbili hasimu, genge la Daesh pia limevuruga usalama Libya
Siku 10 zilizopita, watu zaidi ya 100 waliuawa katika mapigano mengine kati ya makundi hayo hasimu, yaliyofanyika baada ya kikosi cha jeshi kutoka mji wa magharibi mwa Misrata kuvamia kituo cha jeshi kilichoko katika mji wa Brak Al-Shati.
Mapigano hayo yanajiri katika hali ambayo, mapema mwezi huu, Khalifa Haftar, Mkuu wa Jeshi la Libya mashariki mwa nchi hiyo na Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya walikutana mjini Abu Dhabi, Imarati na kufikia makubaliano kuhusu utatuzi wa hitilafu za pande hizo mbili. Viongozi hao wawili walikubaliana pia kuunda jeshi moja na kusimamia kwa pamoja uchaguzi wa Rais na Bunge katika kipindi cha miezi sita ijayo.

No comments:

Post a Comment