Sunday, May 21, 2017

SABABU TATU ZA KUMALIZIKA MAZUNGUMZO YA GENEVA 6 BILA KUFIKIWA NATIJA

Mazungumzo ya Geneva sita juu ya mgogoro wa Syria, ambayo yalifanyika chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, yamemalizika bila kufikiwa natija iliyotarajiwa kwa ajili ya kukomesha mgogoro wa nchi hiyo.
Mazungumzo ya Geneva sita yalianza kuanzia tarehe 16 ya mwezi huu na kuhitimisha shughuli zake siku nne baadaye. Mazungumzo hayo yalijikita katika nukta nne muhimu, kupambana na ugaidi, kujitawala, katiba na uchaguzi. Pamoja na hayo mazungumzo ya Geneva sita kama yalivyokuwa mazungumzo mengine ya Astana, hayakuwa na faida kwa ajili ya kutatua mgogoro wa taifa la Syria. Tatizo la kwanza lililoibuka katika mazungumzo ya Geneva sita ni kwamba hayakujikita katika maudhui moja maalimu.
Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria
Kwa mfano tu Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria yeye alitaka kufanyike mazungumzo kuhusiana na katiba ya mustakbali wa nchi hiyo, huku serikali ya Damascus nayo ikikubaliana na pendekezo hilo la mjumbe wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo makundi ya upinzani yalitaka kabla ya lolote lile, kusimamishwa kwanza mashambulizi ya jeshi la Syria. Pamoja na hayo, mafanikio kidogo sana yalifikiwa hasa juu ya kuanza vikao vya wataalamu baina ya Umoja wa Mataifa na upande wa Syria katika uwanja wa kujadili katiba na masuala mengine ya kisheria ambayo yalisisitizwa pia na Staffan de Mistura. Ama suala jingine ni kwamba, kiwango cha maudhui ambazo zilitakiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya Geneva sita zilikuwa nyingi.
Magaidi waliamua kukimbia baada ya kuzidiwa na kuacha zana zao
Kwa mfano mwingine ni kwamba, suala la katiba ni lenye umuhimu mwingi ambapo kila upande linaupa mazingatio maalumu. Kiujumla ni kwamba kuhusiana na katiba kuna njia tatu ambazo ni kuifanyia marekebisho, kuisimamisha na kuibadilisha, suala ambalo bila shaka pande zote zina msimamo unaotofautiana. Na ili kufikiwa makubaliano kuhusiana na masuala hayo kutahitajia muda mwingi zaidi. Kwa ibara nyingine ni kwamba, kila suala lenye taathira ya mazungumzo katika kugawana madaraka, ndivyo ambavyo huwa na umuhimu zaidi huku njia za kufikiwa makubaliano juu yake zikiwa ngumu vile vile.
Mazungumzo yakiendelea mjini Geneva, Uswis
Nukta nyingine ni hii kwamba, kivuli cha upande wa Marekani katika kukwamisha mazungumzo kuhusiana na mgogoro wa Syria, bado kinaendelea kushuhudiwa katika mwenendo huo. Kuhusiana na hilo, ni kwamba katika hali ambayo ujumbe unaoiwakilisha serikali ya Damascus na makundi ya upinzani chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa yalikuwa yakiendelea na mazungumzo yao ya mjini Geneva, ndege za muungano unaoongozwa na Marekani, zilishambulia msafara wa kijeshi wa serikali ya Syria, kitendo ambacho kilitajwa na Bashar Jaafar, mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa kuwa ni aina ya ugaidi wa kimataifa.
Kikao cha Syria huko Astana, Kazakhstan
Ukweli ni kwamba, kwa upande mmoja Marekani ilitekeleza kitendo hicho cha kijeshi na kilicho kinyume na sheria ili kuyapa matumaini makundi ya kigaidi kwamba, Washington bado inayaunga mkono magenge hayo na kwamba yasiwe na wasi wasi wowote juu ya kuvunjika mazungumzo hayo. Na kwa upande mwingine ni kwamba, hujuma hiyo ilisaidia kufelisha mazungumzo yanayoendelea kuhusiana na mgogoro wa taifa hilo la Kiarabu. Hata hivyo na licha ya matatizo yote hayo, na kwa mujibu wa pendekezo la Staffan de Mistura, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria, imepangwa kufanyika mazungumzo ya Geneva saba kuhusiana na mgogoro wa nchi hiyo katikati ya mwezi Juni mwaka huu.

No comments:

Post a Comment