Monday, May 22, 2017

KUENDELEA SIASA ZA KUPENDA VITA ZA MAREKANI KATIKA PENINSULA YA KOREA

Katika hali ambayo baadhi ya duru za habari zimearifu kupungua misimamo ya pande mbili kuhusiana na mgogoro wa Peninsula ya Korea, yaani Marekani na Korea Kaskazini, Washington imetuma meli yake ya kivita aina ya USS Ronald Reagan katika maji ya karibu na Korea Kaskazini.
Kabla ya hapo pia Marekani ilituma meli ya USS Carl Vinson kwenda katika maji ya Peninsula ya Korea suala ambalo lilisababisha kuongezeka mvutano katika eneo hilo. Korea Kaskazini iliitaja hatua ya kutumwa meli hiyo katika maji ya eneo hilo kuwa ni sawa na kutangaza vita huku ikiionya vikali Washington kutokana na madhara makubwa yanayoweza kutokea kufuatia hatua hiyo ya kichokozi. Mbali na Pyongyang, Uchina pia ilikutaja kupenda vita kwa Washington katika eneo hilo kuwa kunatokana na siasa za kiuhasama za baharini ambapo ilimtaka Rais Donald Trump wa Marekani kuachana na mwenendo huo.
Kiongozi wa Korea Kaskazini akikagua marubani wa kike
Kwa kuzingatia indhari za mara kwa mara za Korea Kaskazini juu ya utumwaji wa meli zaidi ya vita katika maji yake, hivyo kitendo hicho cha Washington si cha kustaajabisha sana. Kuhusiana na suala hilo kuna nukta kadhaa za kufaa kuashiriwa. Kwanza ni kuwa, kutumwa meli zaidi za kivita za Marekani katika eneo kunabainisha nafasi athirifu za kimtazamo na siasa za majenerali wa jeshi la nchi hiyo kwa nafasi yao ya kimaamuzi katika ikulu ya nchi hiyo White House. Hata hivyo suala hilo halihusiani tu na eneo pekee la Peninsula ya Korea na mashariki mwa Asia, bali linashuhudiwa pia nchini Afghanistan, Syria, Iraq na Yemen, ambapo makamanda wa jeshi la Marekani wanahusika na kupanga ratiba za kuongeza majeshi ya nchi hiyo ndani ya mataifa hayo.
Meli ya kivita ya Marekani iliyoamuriwa kwenda katika maji ya karibu ka Korea Kaskazini
Amma nukta ya pili ni kwamba, baadhi ya wachambuzi wa mambo wameitaja hatua ya Marekani ya kutuma meli ya USS Ronald Reagan katika maji ya Peninsula ya Korea kuwa yenye shabaha ya mwisho ya Washington kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufanya mazungumzo na Pyongyang. Hii ni kusema kuwa hadi hivi sasa Pyongyang na Washington zimejiandaa kufanya mazungumzo kwa masharti maalumu, hivyo kitendo cha Marekani cha kuendelea kutuma zaidi meli zake za kivita katika maji hayo ni aina fulani ya kuandaa mazingira kwa ajili ya kuisukuma Korea Kaskazini kwenye meza ya mazungumzo. Pamoja na hayo inaonekana kwamba, Moon Jae-in rais mpya wa Korea Kusini haoni kitendo cha kutunishiana misuli baina ya Korea Kaskazini na Marekani kama kinaweza kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya pande mbili. Na ni kwa ajili hiyo ndio maana akautaka Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Seoul, usaidie katika utatuzi wa mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea.
Moon Jae-in, Rais Mpya wa Korea Kusini
Katika mazungumzo ya simu na António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini, sambamba na kusisitizia suala hilo, alisema kuwa, kuhitimishwa mgogoro wa eneo la Peninsula ya Korea kunahitajia ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Korea Kusini. Suala hilo linaonyesha kwamba, serikali Seoul ambayo inahesabika kuwa muitifaki mkubwa wa Washington, haikubaliani na siasa za Marekani kuhusiana na eneo hilo kama ambavyo inazitambua siasa hizo kuwa ndizo zinazochafua usalama wa eneo hilo. Marekani pia inafahamu vyema kwamba, mgogoro wa Peninsula ya Korea ikiwa hautatatuliwa kwa njia za kisiasa na badala yake zikatumika njia za kijeshi, basi utasababisha maafa makubwa. Hata kama kwa upande wa usalama, Marekani inaonekana iko mbali na Peninsula ya Korea, lakini kambi zake za kijeshi zilizoko Korea Kusini na Japan zitakuwa za kwanza kuangamizwa na makombora ya Korea Kaskazini. Ni kwa ajili hiyo ndio maana makamanda wa jeshi la Marekani hawapendelei kumaliza mgogoro wa eneo hilo kwa njia za kijeshi.
Kim In Ryong, Naibu Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa
Pamoja na hivyo, makamanda wa nchi hiyo wanadai kuwa, kuongezeka mvutano wa eneo hilo kumeilazimisha Washington kutuma zana za baharini katika maji ya eneo zikiwemo meli za kivita kwa shabaha ya kufanya doria. Suala hilo lina maana kwamba, Marekani inatumia mgogoro huo kwa ajili ya kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo kwa nia ya kuzidi kuizingira China. Wakati huo huo, naibu balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, sasa umefika wakati Marekani kuachana na siasa zake za uhasama dhidi ya Pyongyang. Kim In Ryong amesema kuwa, kabla ya Marekani kuanza mazungumzo yoyote na Korea Kaskazini, kwanza inatakiwa kuachana na siasa zake za uadui dhidi ya nchi yake.

No comments:

Post a Comment