Tuesday, May 23, 2017

MALALAMIKO YA WAYEMEN KWA KIGUGUMIZI CHA UMOJA WA MATAIFA

Wakazi wa mji mkuu wa Yemen Sana'a wamefanya maandamano sambamba na safari ya Ismail Ould Sheikh Ahmad, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen mjini humo na kutaka kuhitimishwa mzingiro wa pande zote dhidi ya nchi hiyo.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu wamelaani vikali kimya cha kutia aibu cha Umoja wa Mataifa mkabala na matatizo na masaibu ya wananchi wa Yemen na hatua ya umoja huo ya kutochukua hatua za kivitendo katika uwanja huo. Ismail Ould Sheikh Ahmad, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen Jumatatu ya jana aliwasili mjini Sana'a kwa shabaha ya kukutana na makundi ya nchi hiyo lengo likiwa ni kuandaa mazingira ya kufanyika duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Yemen.
Katika mazingira kama haya, msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa, madhali Umoja wa Mataifa hauna uwezo wa kufanya chochote, kukutana na wawakilishi wa umoja huo ni hatua isiyo na maana wala faida yoyote. Isipokuwa kama Umoja wa Mataifa utabadilika na kufungamana na ubinadamu, maadili na kufanya kazi kwa mujibu wa majukumu yake. Muhammad Abdul-Salam, msemaji wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen alitangaza hapo jana kwamba, tajiriba inaonyesha kuwa, Umoja wa Mataifa huchukua hatua pale madola makubwa yanapotaka umoja huo uchukue hatua. Abdul-Salam ameongeza kuwa, wananchi wa Yemen wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu hivi sasa lakini Umoja wa Mataifa umefumbia macho hilo.
Ndege za kijeshi za Saudia huishambulia Yemen kila siku
Saudia ikipata himaya ya Marekani ilianzisha hujuma dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutoroka nchi. Kwa kuzingatia faili la utendaji dhaifu wa Umoja wa Mataifa katika kutatua migogoro mbalimbali ulimwenguni si ajabu kuona umoja huo ukiathirika na lobi za Wasaudia na kubadilisha misimamo yake badala ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuwa upande wa wananchi wanaotaabika wa Yemen. Ni katika mazingira haya ndipo Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa akaitoa Saudia katika orodha nyeusi ya nchi zinazofanya mauaji dhidi ya watoto, hatua ambayo ilifuatiwa na maswali mengi hasa kutokana na kuwa wadhiha jinai za Aal Saud dhidi ya watoto wa Yemen.
Kigugumizi cha Umoja wa Mataifa mkabala na mauaji ya umati dhidi ya wananchi wa Yemen yanayofanywa na utawala wa Aal Saud na mamluki wake linahesabiwa kuwa jambo hatari mno ambalo kimsingi linakinzana bayana na majukumu na malengo ya umoja huo. Hatua hizo za Umoja wa Mataifa zimeifanya taasisi hiyo ya kimataifa ihesabiwe kuwa mshirika wa jinai za Saudia huko Yemen. Kwa mwenendo huo, Umoja wa Mataifa haujakuwa na utendaji unaotakiwa mkabala na mgogoro wa Yemen na kwa msingi huo haujaweza kuzuia jinai za utawala wa Aal Saud huko Yemen.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua pekee iliyochukuliwa na Umoja wa Mataifa na ambayo inatazamwa kwa jicho zuri na walimwengu ni juhudi za mwakilishi wake maalumu katika masuala ya Yemen za kuitisha mazungumzo ya kitaifa, hatua ambayo nayo haikuweza kufunika kigugumizi cha umoja huo katika mgogoro wa nchi hiyo. Hata hivyo, hatua hiyo nayo haijawa na msaada wowote katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen.
Kuna maswali mengi kuhusiana na utendaji wa Ismail Ould Sheikh mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen na kwa mujibu wa fikra za waliowengi nchini humo ni kwamba, afisa huyo wa UN amekuwa na nafasi katika njama na katika kuifanya hali ya nchi hizo izidi kuwa mbaya. Hii ni kutokana na kuwa, misimamo yake imekuwa ikilenga zaidi katika kufunika hatua za ugombanishaji na uzushaji migogoro za Saudia. Mazingira yaliyowekwa na Saudia na waungaji mkono wake, nayo yameifanya mipango iliyopendekezwa na Ould Sheikh kutokuwa ya uwiano na kivitendo kuwa ni ya kupendelea upande mmoja. 
Mazingira haya yameifanya safari ya Ismail Ould Sheikh mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen huko Sana'a isipokelewe vizuri na wananchi pamoja na viongozi wa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment