Mamilioni ya raia wa Nigeria wanakabiliwa na
baa la njaa hasa katika maeneo ambayo yana ukosefu wa amani kutokana na
mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.
Ripoti zinaonyesha kuwa, karibu
raia milioni tano wa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria
wanakabiliwa na baa la njaa na wanaishi kwa kutegemea misaada ya
chakula. Mashirika ya kieneo na kimataifa ya utoaji misaada ya
kibinadamu yanasema kuwa, yamekuwa yakikabiliwa na changamoto nyingi
katika ufikishaji misaada kwa walengwa likiwemo suala la ukosefu wa
usalama na kuibiwa misaada hiyo kabla ya kuwafikia watu wenye shida nao
kubwa.
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa
Umoja wa Mataifa, Toby Lanzer hivi karibuni alitangaza kuwa, watu
wanaokadiriwa milioni saba katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa
Nigeria wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa na kwamba wanadhamini mlo
mmoja kwa siku kwa tabu kubwa.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha
kuwa, kuna wasiwasi kwamba kundi la kigaidi la Boko Haram litawazuia
raia kulima mazao ya chakula baada ya kukosa kulima kwa misimu mitatu
mfululizo na kwamba suala hilo litazidisha hali mbaya katika maeneo ya
kaskazini mwa Nigeria na kandokando ya Ziwa Chad.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, watu
wawili kati ya kila watatu miongoni mwa wakazi milioni 10.7 wa kaskazini
mwa Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu.
No comments:
Post a Comment