Wanajeshi wanne wa Misri wameuawa baada ya gari lao kulengwa kwa bomu katika Peninsula ya Sinai.
Duru za kijeshi zimearifu kuwa, mlipuko huo ulitokea yapata
kilomita 20, kusini mwa mji wa al-Arish, kaskazini mwa eneo la Sinai.
Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa katika
shambulizi hilo la bomu, linaloaminika kufanywa na magenge ya kigaidi
yanayofungamana na kundi la kitakfiri la Daesh.
Shambulizi hilo la jana limefanyika siku mbili baada ya hujuma
nyingine kama hiyo ya bomu kuua askari 10 wa jeshi la Misri katikati mwa
Peninsula ya Sinai. Hata hivyo, vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya
kaskazini mwa Afrika vilifanikiwa kuangamiza magaidi 15 katika
operesheni hiyo, mbali ya kuwatia mbaroni wengine 7.
Eneo la Sinai Kaskazini limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara
kwa mara ya kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la kigaidi la
Daesh nchini Misri, hujuma zilizoshadidi baada ya kundi hilo kutangaza
utiifu kwa kundi la kigaidi la Daesh mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment