Friday, March 10, 2017

UN YATAKA KUTUMWA ASKARI WENGINE WA KIMATAIFA DRC

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kutuma askari wengine 320 wa kofia buluu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
António Guterres alitoa mwito huo jana Ijumaa kwenye ripoti yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na sambamba na kuelezea kusikitishwa sana na kuongezeka uvunjaji wa haki za binadamu nchini humo, ametaka kuongezewa nguvu kikosi cha kimataifa cha kulinda amani MONUSCO ili kiweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwalinda raia.
Katika ripoti yake hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha ametaka vikosi vingine viwili vitumwe katika miji ya Lubumbashi na Katanga ili kuzuia miji hiyo kukumbwa na machafuko wakati wa uchaguzi ujao.
Aidha amesisitiza kuwa, mwaka 2017 ni mwaka muhimu mno kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kikosi cha kulinda amani wa Umoja wa Mataifa DRC

Amesema, kikosi cha MONUSCO kinafanya kazi kubwa nchini humo na inabidi kiendelee kuwepo kwa ajili ya kusimamia mchakato wa kisiasa na kulinda mafanikio yaliyopatikana hadi hivi sasa katika jitihada za kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Kazi kuu ya askari wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo ni kuwalinda raia na wako nchini humo tangu mwaka 1992 chini ya mwavuli wa kikosi cha MONUSCO ambacho hivi sasa kina takriban wanajeshi 19 elfu wa kofia buluu kutoka nchi mbalimbali duniani.

No comments:

Post a Comment