Sunday, March 26, 2017

IRAN YATAKA MAREKANI ISHTAKIWE KWA JINAI ZA KIVITA BAADA YA MAUAJI YA MOSUL

Afisa wa ngazi za juu nchini Iran amesema kuwa, hujuma za ndege za kivita za Marekani katika mji wa Mosul, Iraq ambazo zimeua idadi kubwa ya raia, ni jinai za kivita.
Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, jinai iliyofanywa na Marekani huko Mosul ni sawa na jinai za kivita zinazofanywa na magaidi wa Daesh (ISIS) pamoja na makundi mengine ya magaidi wakufurishaji ambao wanawalenga raia na watu wasio na hatia. Amesema jinai hizo za Marekani zinapaswa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo katika mahakama ya kimataifa.
Siku ya Jumamosi Marekani ilikiri ilifanya mashambulizi ya angani huko magharibi mwa Mosul mnamo Machi 17 mwaka huu na kuua raia 200. Wakuu wa Iraq wanasema Mareknai ilifanya hujuma kadhaa siku hiyo.
Maeneo ya raia yaliyohujumiwa na Marekani huko Mosul, Iraq
Shamkhani amesema, hata kama Marekani inadai eti hujuma hiyo haikuwa ya makusudi, lakini hilo haliwaondoi hatiani Wamarekani waliotenda jinai hiyo. Shamkhani amesema, jeshi la Marekani limekuwa likiua raia wasio na hatia katika eneo hili kwa kisingizo cha kupambana na ugaidi.
Umoja wa Mataifa pia umetangaza kushtushwa na kupoteza maisha raia katika shambulio hilo la Marekani mjini Mosul, kaskazini mwa Iraq.

No comments:

Post a Comment