Friday, March 17, 2017

SERIKALI YA SUDAN KUSINI YALAUMIWA KWA KUSABABISHA BAA LA NJAA

Serikali ya Sudan Kusini ndiyo inayobeba lawama kubwa kwa baa la njaa linaloshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.
Hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa katika kipindi hiki ambapo mgogoro wa kibinadamu unaoisumbua nchini huyo unakaribia kuwa maafa makubwa ya kibinadamu. 
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema: Serikali ya Sudan Kusini ndiyo inayobeba lawama kubwa kwa baa la njaa linaloshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo huku Rais wa nchi hiyo Salva Kiir akiendelea kutumia mamilioni ya dola zinazotokana na mauzo ya mafuta kuimarisha vikosi vyake vya ulinzi.
Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini yanakabiliwa na baa la njaa na kwamba karibu nusu ya jamii ya watu wa nchi hiyo yaani karibu watu milioni tano na laki tano, wanasumbuliwa na uhaba wa chakula. 
Raia wanaosumbuliwa na njaa Sudan Kusini
Ushahidi unaonesha kuwa, baa hilo la njaa linatokana na machafuko na vita hususan katika jimbo la Unity, hatua ya jeshi la serikali ya kuwazuia watoa misaada ya kibinadamu kufika kwenye maeneo yenye njaa na kukimbia raia kutokana na mapigano ya ndani. Umoja wa Mataifa unasema kwa uchache nusu ya raia wa Sudan Kusini wamelazimika kuwa wakimbizi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. 
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la mapinduzi. Japokuwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2015 yalizidisha matumaini ya kuhitimishwa vita vya ndani lakini machafuko yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yamezusha tena wasiwasi mkubwa na kusababisha matatizo mengi kwa raia wa kawaida. Makubaliano hayo ya amani pia yamefutiliwa mbali baada ya kiongozi wa  waasi, Riek Machar kukimbilia nje ya nchi.
Hata hivyo kukimbia kwa Machar hakukuhitimisha vita vya ndani nchini Sudan Kusini na ripoti mbalimbali zinasema jeshi linalodhibitiwa na Rais Salva Kiir limekuwa likifanya mauaji ya kikabila. Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia imethibitisha kuwa, mauaji ya kimbari yanafanyika nchini Sudan Kusini lakini hadi sasa hakujachukuliwa hatua madhubuti za kukomesha hali hiyo.
Salva Kiir na Riek Machar
Sambamba na hayo Sudan Kusini inasumbuliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Mamilioni ya raia wanaishi kama wakimbizi katika maeneo ya mpakani au kwenye nchi jirani, na wengi miongoni mwao wanasumbuliwa na uhaba wa chakula na huduma za afya. Mashamba ya kilimo yameharibika na wakulima wengi wanalazimika kuishi katika kambi za wakimbizi.
Takwimu zinaonesha kuwa, sasa asilimia 42 ya watu wote wa Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na matatizo hayo ya kiuchumi, vita vya ndani na kusambaratika kwa sekta ya kilimo.
Mgogoro wa Sudan Kusini kwa upande mwingine unachochewa zaidi na uingiliaji wa madola ya kigeni ambayo yananyonya maliasili na utajiri wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Pato la mafuta la nchi hiyo sasa linatumika kununua silaha kutoka kwa makampuni makubwa ya nchi za Magharibi ambazo hapana shaka kuwa hazitaki au kwa uchache hazipendelei kuona soko la silaha za zana za kivita la Sudan Kusini likitoweka kwa kupatikana amani na utulivu nchini humo. 
Jeshi la Sudan Kusini linatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari
Ni kweli kwamba kwa sasa nchi kadhaa za Afrika zinasumbuliwa na baa la njaa, lakini pia hatuwezi kukanusha kwamba, utendaji mbaya wa viongozi wa Sudan Kusini umechangia sana katika kuzidisha hali mbaya ya sasa nchini humo. Baya zaidi ni kuwa, viongozi wa Serikali ya Sudan Kusini wanawazuia wafanyakazi wa jumuiya ya misaada ya kibinadamu kufika katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Kwa msingi huo inathibitika kuwa, mgogoro wa sasa wa Sudan Kusini ni matokeo ya siasa mbaya za viongozi wa nchi hiyo zinazosababisha maafa makubwa kwa raia wa kawaida, na jamii ya kimataifa inalazimika kuchukua hatua madhubuti zaidi za kukabiliana na viongozi kama hao wasiowajibika. 

No comments:

Post a Comment