Friday, March 17, 2017

KANSELA WA UJERUMANI ANGELA MERKEL KUKUTANA NA DONALD TRUMP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kukutana na rais wa Marekani Donald Trump kwa mara ya kwanza mjini Washington. Mazungumzo yao yatajikita juu ya sera yenye utata ya Rais Trump ya 'Marekani kwanza',  
Angela Merkel und Donald Trump (picture-alliance/dpa/M. Kappeler/R. Sachs)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwenyeji wake rais Donald Trump wanatarajiwa kujadili uhusiano baina ya nchi zao na juu ya uhusiano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya kama mshirika wa Marekani katika biashara, usalama na maadili ya kimsingi.  Kwa mujibu wa duru za serikali ya Ujerumani Kansela Merkel pia anataka kujadili na mwenyeji wake, migogoro ya Syria, Libya, hali ya nchini Afghanistan na mgogoro wa nchini Ukraine. Maswala mengine ni uhusiano na Urusi, harakati za kupambana na ugaidi na sera juu ya wakimbizi.  Hata hivyo wachunguzi wanasema huenda swala jingine muhimu likawa msimamo wa rais Donald Trump juu ya kuyaweka mbele maslahi ya nchi yake na mtazamo wake juu mikataba ya biashara na jinsi inavyohusiana na uchumi wa Marekani. 
Mwakilishi wa Ujerumani anayesimamia kamati ya Ulaya inayoshughulikia uhusiano na nchi za nje Josef Janning amesema siasa za Marekani hazijawahi kuwa za kutatanisha kama ilivyo sasa.  Kwa upande wake Profesa John Harper wa chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Bolgna na mtaalamu wa sera za nje za Marekani amesema kansela Merkel atapaswa kutafuta njia mpya ya kujaribu kuanzisha uhusiano wa kikazi na rais Trump. Profesa huyo amesema rais Trump anatofautiana sana na marais wa Marekani wa hapo awali Barack Obama na George Bush kwa sababu Trump hakuwa na uzoefu wa kuendesha  serikali kabla ya kuwa rais.
Deutschland Angela Merkel, Spitzengespräch der deutschen Wirtschaft in München (picture-alliance/Geisler-Fotopress) Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Viongozi hao wanatofautiana sana katika mitazamo ya siasa za dunia; kwa mfano Kansela anapendelea ushirikiano na nchi nyingine katika kuzikabili siasa za dunia wakati Trump kama anavyoendelea kubainika anaonyesha kupendelea mtazamo wa taifa kubwa katika kuyakabili maswala ya kimataifa. Trump anapuuza ushirikiano na taasisi za kimataifa na badala yake anazingatia siasa kwa mtazamo wa mashindano.
Bwana Josef Janning amesema lengo la Kansela Merkel ni kupata angalau kauli thabiti ya rais Trump juu ya mchakato wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi  G-20 na juu ya haja ya kuyashughulikia maswala kwa njia ya ushirikiano. Naye Profesa Harper anasema anatumai kuwa Kansela Merkel atafanikiwa kumshawishi rais Trump aache kuushutumu Umoja wa Ulaya na pia aache kuwaendekeza wanasiasa kama Marine le Pen wa Ufaransa. Ni vigumu kubainika katika mkutano wa kwanza wa viongozi wa Ujerumani na Marekani iwapo watakubaliana msingi wa kufanya kazi kwa pamoja. Hata hivyo kansela wa Ujerumani aliliambia gazeti moja la hapa nchini Ujerumani "Saarbruecker" kwamba wakati wote ni vizuri kujadiliana badala ya kumjadili mtu. Bibi Merkel amesema Ujerumani na Marekani zitanufaika ikiwa zitashirikiana vizuri na kwa haki.

No comments:

Post a Comment