Thursday, March 9, 2017

MAREKANI YAITANGAZIA DUNIA VITA VYA KIBIASHARA

Marekani imetoa tishio la vita vya kibiashara dhidi ya dunia. Waziri wa Biashara wa Marekani Wilbur Ross amesema Marekani imekuwa katika vita vya kibiashara kwa miongo kadhaa lakini sasa nchi hiyo iko tayari kutumia uwezo wake wote kujibu mapigo.
Hivi sasa uchumi wa Marekani unakabiliwa  na nakisi ya bajeti ya takribani dola bilioni 800  huku mlingano wa kibiashara ukiwa ni kwa faida ya madola ya kigeni. Mwaka 2014, kwa kila dola  trilioni moja na bilioni 500 ambazo ni thamani ya mauzo ya nje ya Marekani, nchi hiyo imekuwa ikinunua huduma na bidhaa kutoka nje zenye thamani ya trilioni mbili na dola bilioni 300.
Katika mlingano wa mabadilishano ya kibiashara, China inaiongoza Marekani kwa dola bilioni 340, Umoja wa Ulaya bilioni 142, Japan bilioni 167, Mexico bilioni 53 na Canada bilioni 35. Kwa msingi huo nchi hizo zinauiuzia Marekani bidhaa na huduma zaidi ya Marekani inavyoweza kuziuzia.
Kiu isiyokwisha ya Wamarekani ya kutaka kutumia kwa wingi bidhaa kiholela ni jambo ambalo limepelekea nchi hiyo kukumbwa na wimbi la mmiminiko wa bidhaa za kigeni. Halikadhalika gharama za uzalishaji bidhaa Marekani ziko juu sana ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia; na ni kwa sababu hii ndio maana Wamarekani wanafadhilisha kununua bidhaa za kigeni ambazo zinauzwa kwa bei nafuu.
Bidhaa zikiwasili bandarini
Sheria ngumu za kuajiri wafanyakazi pamoja na mfumo mbaya wa ushuru ni mambo ambayo yamepelekea wazalishaji bidhaa Marekani kutoweza kushindana na wenzao wa kigeni.
Takwimu zinaonyesha kuwa, Marekani ndio nchi yenye uchumi mkubwa duniani na moja ya nchi muhimu zaidi kiviwanda. Pamoja na hayo miongoni mwa sekta 11 muhimu za kiviwanda, Marekani imeweza kufanikiwa katika sekta tatu tu ambazo ni sekta ya dawa, sekta ya plastiki na sekta ya utengenezaji ndege. Katika upande wa pili Marekani inaagiza kutoka nchi zingine duniani bidhaa muhimu kama vile bidhaa za elektroniki, mashine za viwanda, magari na petroli na hivyo kupelekea uchumi wa nchi hiyo kudhoofika.
Hivi sasa kwa kuzingatia matatizo katika muundo wa kiuchumi wa Marekani na uraibu wa kutumia bidhaa kupindukia (consumerism) walionao raia wa nchi hiyo, wakuu wa Washington sasa wanataka kuanzisha vita vya kibiashara na mataifa mengine duniani.
Katika miaka ya nyuma, Marekani pia ilikuwa na ushindani mkubwa na baadhi ya washirika wake wa kibiashara hasa Japan na China. Hivi sasa serikali ya Marekani imeweka kando udiplomasia na imetangaza wazi vita vya kibiashara. Hivi sasa mbali na matokeo tarajiwa ya vita vya kibiashara baina ya madola makubwa duniani, nukta nyingine muhimu ni kuwa, Marekani haiwezi kuibuka mshindi hadi pale itakapo badilisha muundo wake wa kiuchumi na kuweza kudhibiti utamaduni mbovu wa watu wake kutumia bidhaa kiholela na kupita kiasi.
Tab'an Rais Donald Trump amechukua hatua kuekelea katika marekebisho hayo kwa kutoa nara kama vile 'Marekani Ipewe Kipaumbele', 'Nunua Bidhaa za Marekani' , 'Ajiri Mmarekani' n.k. Lakini kuna shaka kubwa iwapo wazalishaji bidhaa, wafanya biashara wakubwa na raia wa Marekani  wataafiki kutekeleza mabadiliko hayo. Ni kwa sababu hii ndio maana badala ya serikali ya Marekani kujikita katika kuleta mabadiliko ndani ya nchi imechukua mkondo wa kuibua utata katika uchumi na biashara ya kimataifa kwa kutumia mabavu ili kujaribu kuzuia kuporomoka kusikoepukika kwa nchi hiyo katika uga wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment