Sunday, March 26, 2017

IRAN KUIWEKEA MAREKANI VIKWAZO

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Is'haq Jehangiri
Kufuatia hatua ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo itachukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuiwekea Marekani vikwazo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Is'haq Jehangiri amesema, serikali ya Iran inachunguza hatua itakazochukua endapo Marekani itakiuka mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango wa Pamoja wa Utekeelzwaji JCPOA.
Jehangiri amesema hata kama vikwazo vipya vya Marekani si ukiukwaji wa JCPOA, lakini Marekani itapoteza itibari yake kimataifa.
Jehangiri amesisitiza kuwa, uchumi wa Iran unazidi kuimarika kutokana na utekelezwaji wa sera za uchumi wa kimapambano na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa umoja na mshikamano imeweza kusimama kidete mbele ya vikwazo vikubwa  zaidi.
Hivi karibuni wajumbe kadhaa wa vyama vya Democrat na Republican katika Baraza la Senate la Marekani walipasisha rasimu ya sheria ya kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran.
Bunge la Congress la Marekani
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, watu na mashirika au taasisi za Iran zitawekewa vikwazo kwa kuhusika na mpango wa makombora ya kujihami ya nchi hii.
Katika kujibu hatua hiyo, Kamati ya Sera za Kigeni na Usalama wa Taifa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, linapanga kuwasilisha mswada wa kulitaja Jeshi la Marekani na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA kuwa taasisi za kigaidi.
Aidha katika hatua ya kujibu kufuatia uhasama na chuki za Baraza la Congress la Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza kuyawekea vikwazo mashirika 15 ya Marekani kutokana na mashirika hayo kuunga mkono jinai na ugaidi wa utawala haramu wa Israel. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mashirika hayo ya Mareknai yamekiuka azimio 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono ugaidi wa Israel. Aidha taarifa hio imelaani muswada huo wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kuutaja kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa.

No comments:

Post a Comment