Thursday, March 9, 2017

MAJIMBO KADHAA MAREKANI YACHUKUA HATUA KUZUIA MARUFUKU MPYA YA TRUMP DHIDI YA WAISLAMU

Amri mpya iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani ya kupiga marufuku raia wa nchi sita za Waislamu kuingia nchini humo imeendelea kupingwa kisheria na majimbo ya nchi hiyo baada ya Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Washington kuungana na jimbo la Hawaii kuchukua hatua ya kuzuia utekelezaji wake.
Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Washington Bob Ferguson, ambaye alikuwa mtu wa mwanzo kukwamisha amri ya marufuku ya kwanza iliyotangazwa na Trump amesema, amri mpya ya sasa pia inakiuka Katiba ya Marekani kwa kuwa "haiutendei ipasavyo Uislamu".
Amesema hoja iliyowasilishwa na ofisi yake inataka zuio dhidi ya amri ya mwanzo iliyotangazwa na rais wa Marekani mnamo mwezi Januari litekelezwe pia kuhusiana na dikrii yake mpya.
Hii ni katika hali ambayo Wanasheria Wakuu wa majimbo ya New York, Massachusetts na Oregon wametangaza kuwa nao pia wameshachukua hatua ya kujiunga na shauri la kisheria lililowasilishwa mahakamani na jimbo la Washington pamoja na Minnesota kupinga marufuku iliyotangazwa na Trump.
Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Washington, Bob Ferguson
Amri hiyo mpya iliyotangazwa siku ya Jumatatu baada ya kufanyiwa marekebisho na ambayo inatarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 16 mwezi huu inapiga marufuku kutoa viza za kuingia Marekani watu wanaotoka Syria, Iran, Somalia, Libya, Sudan na Yemen na kufunga kwa muda wa siku 120 mpango wa Marekani kwa ajili ya wakimbizi.
Mwanasheria Mkuu wa Oregon Ellen Rosenblum amesema amri hiyo ya Rais wa Marekani imeathiri jimbo hilo, wakaazi wake, waajiri, taasisi za elimu, mfumo wa huduma za afya pamoja na uchumi.
Mwanasheria Mkuu wa jimbo la New York Eric Schneiderman amesema, kwa jina jingine amri hiyo ni "marufuku dhidi ya Waislamu"
Shauri la kisheria lililowasilishwa na jimbo la Hawaii limeeleza kuwa amri ya Trump itaathiri jamii ya Waislamu wa jimbo hilo, utalii pamoja na wanafunzi wa kigeni…/

No comments:

Post a Comment