Sunday, March 25, 2018

WASI WASI WAMAREKANI KUHUSIANA NA VITA VYA KIBIASHARA KATI YA NCHI YAO NA CHINA

Wasi wasi wa Wamarekani kuhusiana na vita vya kibiashara kati ya nchi yao na China
Suala la Rais Donald Trump wa Marekani kutia saini dikrii ya kupandishwa ushuru wa forodha wa biadhaa za China, limeibua tofauti kubwa za kibiashara kati ya Marekani na China.
Kufuatia hatua hiyo, raia hususan wakulima wa Marekani wamekumbwa na wasi wasi mkubwa juu ya hatua zinazoweza kutekelezwa na China katika uga wa kibiashara. Wasi wasi huo umeibuka baada ya radiamali ya China ya kutangaza kwamba Beijing haitorudi nyuma katika mwenendo huo. Kwa kuzingatia hali mbaya ya uchumi wa Marekani kwa sasa hususan katika sekta ya kilimo, weledi wengi wanaamini kwamba, uzalishali ndio njia pekee inayoweza kuiokoa nchi hiyo kutokana na hali mbaya.
Marais wa China na Marekani
Hata hivyo kwa kutiwa saini dikrii hiyo na kadhalika hatua mkabala za Wachina katika uwanja huo, kunaifanya njia ya wokovu kufungwa na hivyo kuisababishia matatizo zaidi ya kiuchumi jamii ya Marekani. Kufuatia hali hiyo, Cui Tiankai, balozi wa China mjini Washington sambamba na kuonyesha kutofurahishwa na maamuzi ya serikali ya Marekani kuhusiana na kadhia hiyo amesema kuwa, kamwe China haikupendelea kuingia katika vita vya kibiashara na Marekani, lakini akatahadharisha kwamba, iwapo Beijing italazimika kuingia katika uwanja huo, basi haitorudi tena nyuma. Radiamali hiyo kali ya China, imeisababishia wasi wasi mkubwa jamii ya kiuchumi ya Marekani kiasi cha kuyafanya masoko ya hisa nchini humo kuporomoka.
Mgogoro kati ya Marekani na China
Timu ya Rais Donald Trump wa Marekani inaamini kwamba, kuzidishwa ushuru wa forodha kwa bidhaa za China kwa kiasi fulani kutapelekea kushuka kwa nakisi ya kibiashara ya Marekani ambapo licha ya kuwa huenda suala hilo likawa na madhara kwa sekta tofauti za kiuchumi nchini, lakini kwa muda mrefu litakuwa na maslahi kwa uchumi na jamii nzima ya Marekani. Peter Navarro, mshauri mkuu wa rais katika masuala ya biashara na viwanda, anasema kuwa, kupungua nakisi ya kibiashara, ni jambo linalotishia usalama wa taifa na kuifanya nchi hiyo kutegemea madeni na uwekezaji wa kigeni. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kutekelezwa dikrii hiyo mpya ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa mashirika makubwa kama vile Boeing na Apple, kutakuwa na madhara makubwa sambamba na kupelekea makumi ya maelfu ya watu kupoteza fursa zao za kazi ndani ya nchi hiyo. Kadhalika iwapo China itachukua hatua ya kulipiza kisasi, basi sekta ya kilimo ya Marekani hususan uzalishaji wa mazao ya Soya, nao utaathirika zaidi huku makumi ya maelfu ya watu pia wakipoteza ajira. 
Mvutano ukiendelea
Jim Byrum, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Marekani, anasema: "Hivi sasa tunashuhudia mgogoro mkubwa. Ninachukia hata kutamka neno 'vita vya kibiashara,'  hata hivyo inaonekana kuwa sisi tayari tumesukumwa kuelekea upande huo." Mwisho wa kunukuu. Inaonekana kuwa, vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinakaribia kutokea. Ni wazi kuwa kupungua uzalishaji ni moja ya matokeo ya siasa ambazo zitasababisha kuongezeka kiwango cha watu wasio na ajira nchini Marekani. Kwa hakika wasi wasi wa mashirika na wakulima wa Marekani ni jambo lililo mahala pake, kwani hatua mkabala ya Wachina itazisababishia madhara makubwa sekta tofauti za kiuchumi nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment