Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri
ametangazwa mshindi wa uchaguzi tata wa rais uliofanyika Jumatatu
iliyopita, kwa kuzoa asilimia 92 ya kura zote zilizopigwa.
Uchaguzi wa Rais wa Misri uliofanyika kwa siku tatu kuanzia
tarehe 26 Machi, ulimalizika juzi tarehe 28. Katika uchaguzi huo al Sisi
alichuana na Moussa Mostafa Moussa wa chama cha al Ghad ambaye ametajwa
na vyombo vya habari kuwa hakuwa mpinzani wa al Sisi bali alichomekwa
kwenye kinyang'anyiro hicho kuhalalisha zoezi hilo.
Mambo mawili yametajwa kuwa sababu kuu za ushindi wa Abdul Fattah al Sisi hata kabla ya uchaguzi huo kufanyika.
Kwanza ni kukandamizwa kambi kuu ya upinzani katika kipindi chote cha
uongozi wa miaka minne iliyopita ya utawala wa al Sisi. Kijadi,
mpinzani mkuu wa kiongozi wa sasa wa Misri alipaswa kuwa mgombea yeyote
wa harakati ya Ikhwanul Muslimin. Katika kipindi chote cha miongo kadhaa
iliyopita watawala wa Misri wamefanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba,
harakati hiyo inakandamizwa, viongozi wake wanaoswekwa jela na wafuasi
wao wanahukumiwa vifungo au hata adhabu ya kifo. Baada ya kuondolewa
madarakani dikteta wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak katika mapinduzi ya
wananchi ya mwaka 2011, harakati hiyo ilipata anga ya pumua kidogo na
mgombea wake akashinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika
nchini humo. Hata hivyo serikali ya Muhammad Mursi haikuishi zaidi ya
mwaka mmoja. Serikali hiyo ya kwanza kuchaguliwa na wananchi kwa njia za
kidemokrasia, iliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi
yaliyoongozwa na Jenerali Abdul Fattah al Sisi.
Sababu kuu ya pili ya ushindi wa al Sisi ni kubinywa na hata
kukamatwa wapinzani mashuhuri wa kiongozi huyo kabla kidogo ya zoezi la
uchabuzi wa rais. Serikali ya Cairo iliwazuia wagombea mashuhuri kama
Ahmad Shafiq, Sami Hafez Anan, Abdel Munim Abul Futuh kujitosa katika
kinyang'anyiro hicho kwa kutumia visingizio mbalimbali. Hata Moussa
Mustafa Moussa aliyechuana na al Sisi katika uchaguzi huo anajulikana
kuwa muungaji mkono wa Abdul Fattah al Sisi.
Uchaguzi wa rais uliofanyika Misri ulifanyika kwa kuwa hakukuwa na
budi kufanyika, na al Sisi alilazimika kuitisha zoezi hilo. Mchambuzi wa
masuala ya siasa Hassan Shukri anasema: Uchaguzi wa rais
uliofanyika Misri haukuwa ushindani baina ya wagombea wawili bali
lilikuwa zoezi la kuhalalisha utawala wa al Sisi. Hata hivyo siasa za
ngumi ya chuma zinazotekelezwa na al Sisi akisaidiwa na jeshi tangu
miaka minne iliyopita, kutotimizwa ahadi zilizotolewa na kiongozi huyo
kwa wananchi na kupuuzwa au kukanyagwa demokrasia na uhuru vimeshusha
chini zaidi imani ya Wamisri kwa kiongozi huyo."
Ni kwa kutilia maanani sababu hizo mbili ndiyo maana Abdul Fattah al
Sisi akaingia kwenye klabu ya viongozi wa nchi za Kiarabu wanaoshinda
chaguzi za rais kwa kupata eti asimia zaidi ya 90 ya kura zilizopigwa!
Pamoja na hayo wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii wanatarajia
kuwa, jenerali huyo mstaafu hatafanya marekebisho ya katiba
yanatakayomruhusu kubakia madarakani baada ya kumalizika muhula wake wa
vipindi viwili kama wafanyavyo baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika na
Kiarabu.
No comments:
Post a Comment