Monday, March 5, 2018

KUONGEZEKA BAJETI YA KIJESHI YA CHINA KATIKA MWAKA 2018

Kuongezeka bajeti ya kijeshi ya China katika mwaka 2018
Serikali ya China imetangaza kuongeza bajeti yake ya kijeshi katika mwaka huu wa 2018.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bajeti ya kijeshi ya China katika mwaka huu wa 2018 itaongezea kwa asilimia 8.10. Bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo imetangazwa kuwa  dola  bilioni 175. Duru za kijeshi nchini China zinasema kuwa bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo bado ni ndogo ikilinganishwa na bajeti ya Marekani ya dola bilioni 700. Pamoja na hayo, hatua ya China ya kuongeza bajeti yake ya kijeshi inahesabiwa kuwa ni aina fulani ya radiamali ya nchi hiyo kwa mipango ya kijeshi ya kichokozi ya Marekani katika eneo la mashariki mwa Asia; ambayo imeshika kasi katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa hivi karibuni wa utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Rais Donald Trump wa Marekani 
Katika stratejia yake mpya ya usalama wa taifa iliyoitangazwa hivi karibuni, Marekani inahisi kuwa China  ni nchi tishio zaidi dhidi yake na inasisitiza kuhitimishwa nguvu hiyo ya China. Moja ya siasa za kistratejia za Marekani mkabala na China ni kuona kunafanyika jitihada za kuishawishi Beijing izidishe bajeti yake ya kijeshi sambamba na kuiingiza katika mashindano ya kijeshi kati yake na Marekani na waitifaki wake katika eneo kama vile Japan na Korea ya Kusini. Siasa ambazo zinatajwa na viongozi wa China kuwa ni siasa za fikra za vita baridi za Washington; na kuamini kuwa Marekani inafanya kila iwezalo ili kuifanya China kuwa na mustakbali kama ule wa Umoja wa Kisovieti. Ndio maana China haipendelei kuingia katika mashindano ya kijeshi na Marekani licha  ya kuzidisha bajeti yake ya kijeshi. 
Nikita Danuk Naibu Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kistratejia ya Russia anasema kuwa: Rais Donald Trump hataki kuharibu misingi ya  ushirikiano kati ya Washington na Beijing. Amejikita zaidi na kuzingatia kubadili ajenda ya siasa za nje za kila siku za Marekani. Nchi hii itaamiliana kwa tahadhari na China na kujaribu kupunguza taathira za China katika eneo. 
Moja ya manowari za China
Pamoja na hayo yote, China inatambua vyema kuwa mipango ya kiuchumi ya Marekani ikiwemo ile ya kuongeza tozo ya ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka China na kuvibana vitega uchumi vya nchi hiyo inaweza kuisababisha madhara nchi hiyo. Ndio maana China nayo hivi karibuni ikaamua kuendeleza mipango yake ya ustawi wa kijeshi yaani kuimarisha uwezo wake wa kujilinda mkabala na  Marekani. Wakati huo huo China inaamini kuwa vita vikuu zaidi vya kulazimishwa dhidi yake kutoka kwa Rais Donald Trump ni vita vya kibiashara na mara kwa mara  imetahadharisha kuhusu madhara ya vita hivyo. 
Majeshi ya China yakifanya maneva kwenye maji ya kusini mwa nchi hiyo
Kwa vyovyote vile  Marekani inafahamu vyema kuwa China ni nchi pekee yenye ushawishi chanya mkabala na nafasi ya kimataifa ya Washington katika maeneo mbalimbali duniani. Suala hilo ndilo lililoifanya Marekani itekeleze siasa za pande zote katika nyanja za kijeshi na kiuchumi dhidi ya Beijing na katika upande wa pili pia serikali ya China inafanya kila iwezalo ili kudhibiti hali ya mgogoro na siasa hizo za Trump; siasa ambazo kwa mtazamo wa Beijing zimefanikiwa na zinaweza kuipelekea kuimarisha amani na usalama katika eneo la mashariki mwa Asia kwa kushirikiana nchi za eneo hilo.

No comments:

Post a Comment