Kwa akali Wapalestina wanane wameuawa shahidi
na wanajeshi katili wa Israel katika maandamano ya Siku ya Ardhi, ya
kulaani hatua ya utawala huo ghasibu ya kupora ardhi zao, yaliyofanyika
leo karibu na uzio wa kibaguzi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imesema mbali na Wapalestina wanane
kuuawa shahidi kwa kumiminiwa risasi na wanajeshi katili wa Israel,
wengine zaidi ya 550 wamejeruhiwa vibaya.
Kituo cha Kutetea Haki za Wapalestina cha Adalah kimelaani vikali
mauaji hayo, na kueleza kusikitishwa kwake na kitendo cha jeshi la
Israel kutumia risasi hai, vifaru na maroketi dhidi ya waandamanaji
ambao hawana ulinzi.
Kituo hicho kimesema mauaji hayo dhidi ya Wapalestina waliokuwa
wakiandamana kutetea ardhi zao zilizoporwa ni kinyume cha sheria za
kimataifa.
Maelfu ya Wapalestina wamejitokeza kushiriki maandamano hayo, licha
ya idadi kubwa ya wanajeshi wa Israel waliojizatiti kwa silaha nzito
kuuzingira uzio huo wa Gaza, na licha ya utawala huo haramu kutumia
fatua za Saudi Arabia kuwashawishi Wapalestina hao kutoshiriki
maandamano hayo.
Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, maandamano ya
kwanza ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi
za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kulaani hatua ya utawala wa
Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina.
Waarabu sita wa Israel ambao hawakuwa wamejizatiti kwa silaha
waliuawa na askari wa Kizayuni katika maandamano hayo yaliyofanyika
Machi 30 mwaka 1976.
No comments:
Post a Comment