Umoja wa Mataifa umetangaza habari ya
kusitisha shughuli zake za utoaji huduma na misaada ya kibinadamu
kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na kuuawa wafanyakazi wake
katika mashambulizi ya hivi karibuni ya magaidi wa Boko Haram.
Taarifa ya Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imesema
kuwa, wahudumu 40 wa UN walikuwa katika mji wa Rann ambao una kambi ya
wakimbizi wa ndani wapatao 55 elfu ulipovamiwa Alkhamisi usiku na
wapiganaji wa Boko Haram.
Amesema kufuatia hujuma hiyo, Umoja wa Mataifa umesimamisha kwa muda
utoaji wa huduma za kibinadamu katika mji huo ulioko kaskazini mashariki
mwa Nigeria.
Siku ya Ijumaa, shirika la madaktari wasio na mipaka lilitangaza
habari ya kusimamisha shughuli zake zote kaskazini mwa Nigeria baada ya
genge la wakufurishaji la Boko Haram kuushambulia mji wa Rann katika
jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Katika shambulizi lililofanywa na genge hilo Alkhamisi usiku, watu 11
wakiwemo wafanyakazi watatu wa kutoa misaada waliuawa huku wengine
watatu wakihofiwa kutekwa nyara baada ya hujuma hiyo.
Mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria na katika nchi
jirani za Chad, Niger, na Cameroon yameshapelekea zaidi ya watu 20 elfu
kuuawa na milioni mbili na laki sita wengine kuwa wakimbizi.
No comments:
Post a Comment