Utafiti mpya wa maoni umeonyesha kuwa, kwa
kila raia kumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanane hawamungi
mkono Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.
Utafiti huo uliofanywa mwezi jana na shirika la utafiti la
Congo Research Group CRG likishirikiana na Kituo cha Utafiri wa Maoni
cha BERCI katika Chuo Kikuu cha New York unaonyesha wazi kuwa, akthari
ya Wakongomani wamechoshwa na uongozi wa miaka 17 wa Rais Kabila na
wangetaka kumuona akiachia ngazi.
Joseph Kabila alikataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula
wake wa utawala kikatiba mwaka 2016, na mpaka sasa hajajitokeza
hadharani kusema iwapo ataachia ngazi baada ya uchaguzi wa rais
unaotazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu au la.
Kwa mujibu wa utafiti huo wa maoni uliowashirikisha Wakongamani elfu
moja katika mikoa yote 26 ya nchi hiyo, asilimia 95 ya waliohojiwa
wanasema wako tayari kushiriki uchaguzi rais wa mwezi Disemba; ambapo
asilimia 26 wanasema wangelimchagua Moise Katumbi, kiongozi wa upinzani
aliyeko uhamishoni, huku asilimia 13 wakisema wangelimchagua mwanasiasa
mwingine wa upinzani Felix Tshisekedi kurithi mikoba ya Kabila.
Utafiti mwingine wa maoni uliofanywa mwaka mmoja uliopita na CRG na
BERCI ulionyesha kuwa, asilimia 38 ya wapiga kura nchini humo wako
tayari kumpigia kura Katumbi, na yumkini kiwango hicho kimeshuka
ikilinganishwa na utafiti wa mwaka huu, kutokana na mwanasiasa huyo
tajiri kutokuweko nchini kwa miaka miwili sasa
No comments:
Post a Comment