Askari polisi watano wa Kenya wameuawa na
wengine watatu kujeruhiwa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi na
kitakfiri la al-Shabaab kushambulia kambi mbili za maafisa usalama
katika mji wa Fino katika kaunti ya Mandera.
Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Laafey huko kaskazini mwa
Kenya, Eric Oronyi amesema shambulizi hilo limefanyika usiku wa kuamkia
leo, ambapo wanamgambo hao wamevamia kituo cha polisi wa kawaida na wa
utawala katika mji wa Fino.
Amesema wavamizi hao kati ya 70 hadi 100 mbali na kutekeleza mauaji
hayo, kadhalika wameng'oa mlingoti wa shirika moja la simu za rununu na
kulemaza mawasiliano.
Mwezi uliopita, maafisa wengine watano wa polisi ya Kenya waliuawa
baada ya wanachama wa al-Shabaab kushambulia msafara wa magari ya
maafisa usalama katika barabara ya Elwak-Kotulo katika kaunti hiyo hiyo
ya Mandera.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye makao yake Somalia mara kwa mara
hutekeleza mashambulizi ndani ya ardhi ya Kenya kuishinikiza serikali
ya nchi hiyo iondoe wanajeshi wake wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda
Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM
No comments:
Post a Comment