Sunday, March 25, 2018

SERIKALI YA NIGERIA INAFANYA MAZUNGUMZO NA BOKO HARAMU YA UWEZEKANO WA KUSITISHA MAPIGANO

Serikali ya Nigeria inafanya mazungumzo na Boko Haram ya uwezekano wa kusitisha mapigano
Waziri wa Habari wa Nigeria amesema serikali inafanya mazungumzo na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano, lengo kuu likiwa ni kuhitimisha kikamilifu uadui na uhasama baina ya pande mbili.
Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa kwa serikali ya Abuja kutangaza kuwa inafanya mazungumzo na Boko Haram kuhusu usitishaji mapigano yaliyosababishwa na uasi uliopelekea kuuawa maelfu ya watu tangu mwaka 2009.
"Wengi wakiwa hawajui, kwa muda sasa tumekuwa tukifanya mazungumzo mapana ya kuhitimisha uhasama na waasi" amesema Lai Mohammed, Waziri wa Habari wa Nigeria kupitia taarifa aliyotoa kuzungumzia pia kilichofanyika hadi kupelekea kuachiwa huru zaidi ya wanafunzi wa kike 100 na kundi la kigaidi la Boko Haram wiki iliyopita.
Wasichana hao walitekwa nyara Februari 19 katika mji wa Dapchi kaskazini mashariki mwa Nigeria. Utekaji nyara huo wa wanafunzi wapatao 110 ulikuwa wa idadi kubwa zaidi tangu wanafunzi wa kike wapatao 270 walipotekwa nyara na kundi la kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Chibok ulioko kaskazini mashariki pia mwa Nigeria mwaka 2014.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria akiwa na wanafunzi wa mji wa Dapchi baada ya kuachiwa huru na kuonana nao mjini Abuja
Siku ya Jumatano iliyopita, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram waliwashangaza wakaazi wa mji wa Dapchi walipoingia na magari mjini humo na kuwaachia huru wasichana hao ambao walisema, wenzao watano walifariki walipokuwa wakishikiliwa na kundi hilo na mmoja mwengine bado hajaachiwa huru.
Kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa Nigeria, makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja kuanzia Machi 19 ndiyo yaliyowezesha Boko Haram kuwaachia huru wasichana hao.../

No comments:

Post a Comment