Thursday, March 22, 2018

KENYA NI MWENYEJI WA WIKI YA KUPAMBANA NA UBAGUZI WA RANGI WA ISRAEL

Kenya ni mwenyeji wa Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel
Duru ya 14 ya 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' inafanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ikijumuisha maonyesho ya filamu, mijadala na matamasha ya kiutamaduni.
Shughuli hiyo ilianza tarehe 12 Machi na itaendelea kwa siku kadhaa zijazo kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) katika utawala haramu wa Israel unaowalenga Wapalestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao.
Filamu kadhaa zinaonyesha kuhusu ubaguzi wa rangi Israel kwa lengo la kuwafahamisha wapenda haki nchini Kenya kuhusu utambulisho wa kibaguzi wa utawala haramu wa Israel. Hafla hizo zimehudhuriwa na watu wa matabaka mbali mbali ya jamii. Mijumuiko ya 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' nchini Kenya imeandaliwa na Harakati ya Mshikamano wa Kenya na Palestina kwa ushirikiano na Tume ya Haki za Binadamu Kenya, Kituo cha Uadilifu wa Kijamii cha Mathare, Kituo cha Utafiti cha Mau Mau, jumuiya za kijamii za Fahamu, Awaaz na Kituo cha Kulinda na Kutetea Haki kati ya taasisi zinginezo.
Kwa ujumla 'Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel' (Israeli Apartheid Week) hulenga kuwahimiza walimwengu kuunga mkono harakati ya kuusisia kwa kila namna utawala haramu wa Israel. Mwaka huu ''Wiki ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi wa Israel'  ilianza Februari 19 na itaendelea hadi tarehe 17 Aprili' katika miji mbali mbali duniani.

No comments:

Post a Comment