Salamu za pongezi alizotoa rais wa Marekani
kwa rais wa Russia kwa ushindi aliopata wa kuchaguliwa tena kuwa rais wa
nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni zimewakasirisha
baadhi ya maseneta nchini Marekani.
Seneta wa chama cha Republican John MacCain amemtuhumu Rais
Vladmir Putin wa Russia kuwa ni dikteta na kusema kwamba: kwa kumpa
salamu za pongezi Vladmir Putin,Trump amewatusi wananchi wote wa
Russia ambao wamenyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi huru na wa
haki ili kuamua kuhusu mustakabali wa nchi yao, ikiwemo idadi kubwa ya
wazalendo wa Russia; watu ambao wamehimili hatari nyingi ili kuweza
kutumia haki yao ya kulalamika na kupambana na utawala wa Putin.
Madai hayo yanatolewa katika hali ambayo katika uchaguzi wa rais wa
Russia uliofanyika hivi karibuni vyama na mirengo tofauti ya kisiasa
ikiwemo ya wapinzani wakubwa wa Kremlin ilishiriki kwenye uchaguzi huo
kuchuana na rais Putin. Hata hivyo kiongozi huyo ameweza kuvutia kura na
mapenzi ya aghalabu ya Warussia kutokana na utendajikazi wake wa miaka
17 hususan mafanikio aliyopata ya kuitatua migogoro ya kisiasa, kiuchumi
na kiusalama iliyotokana na kuvunjika Shirikisho la Kisovieti la Urusi
ya zamani na kufufua tena nguvu na satua ya nchi hiyo katika uga wa
kimataifa. Hali hiyo imetafsiriwa na kuelezewa na mirengo inayoipinga
Russia katika nchi za Magharibi na hasa Marekani kuwa ni udikteta na
hila za kutaka kuyatia mkono matokeo ya uchaguzi wa rais wa Russia
uliofanyika hivi karibuni. Mrengo huo unaitumia kila fursa ikiwemo ya
utoaji salamu za pongezi rais wa Marekani kwa rais wa Russia ili
kuvuruga uhusiano wa Washington na Moscow, ilhali kuwasiliana kwa njia
ya simu marais wa nchi mbili na kupongezana kwa kushinda katika uchaguzi
ni jambo la kawaida na lililozoeleka. Takribani mwaka mmoja na nusu
uliopita Putin alimtumia salamu za pongezi Trump aliposhinda uchaguzi wa
rais wa Marekani uliofanyika mwaka 2016; na hivi sasa baada ya kupita
siku mbili tangu kufanyika uchaguzi wa rais wa Russia, Trump naye
amefanya vivyo hivyo kupitia mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na
Vladmir Putin. Lakini yeye amekwenda hata mbali zaidi kwa kueleza
matumaini aliyonayo ya kupatikana fursa haraka iwezekanavyo ya kukutana
na kufanya mazungumzo na rais wa Russia.
Mrengo unaoipinga Russia nchini Marekani una hofu baada ya kuona
kwamba, licha ya propaganda kali za kueneza sumu dhidi ya Kremlin kwa
kutumia visingizio mbalimbali kama kuingilia Russia uchaguzi wa rais wa
Marekani sambamba na tuhuma mpya dhidi ya Moscow za kumpa sumu jasusi wa
pande mbili wa Uingereza, Trump angali anafanya kila njia ili kuona
uhusiano wa nchi yake na Russia unaboreka.
Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais mwaka 2016 hadi sasa,
rais wa sasa wa Marekani amesisitiza mara kadhaa kwamba bila ya
kushirikiana na Russia baadhi ya mizozo mikubwa ya kimataifa hususan
mgogoro wa vita vya Syria hautoweza kutatuka. Ni kwa sababu hiyo Trump
angali anashikilia msimamo wake wa kuendelea kuwa na mawasiliano binafsi
na rais wa Russia, kitendo ambacho kwa mtazamo wa baadhi ya watu kama
John McCain, mkuu wa kamati ya huduma za vikosi vya ulinzi vya Marekani
katika Seneti ya nchi hiyo, ni dhambi isiyosameheka.
No comments:
Post a Comment