Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama
cha Wanasheria Tanganyika (TLS) nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema
kuwa, kile kinachowapata viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha
Demokrasia na Maendelea (CHADEMA), ni maandalizi ya upinzani huo kuingia
madarakani.
Tundu Lissu ameyasema hayo ikiwa ni baada ya viongozi sita wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti Taifa wa chama Freeman Mbowe,
Katibu Mkuu Vincent Mashinji, Manaibu Katibu Mkuu, John Mnyika (Bara)
na Salum Mwalimu (Zanzibar), Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Chadema
(Bawacha), Esther Matiko na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa, kushtakiwa kwa makosa manane na kisha kunyimwa dhamana.
Kadhalika
Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu,
amefafanua kuwa, kilichowapata viongozi hao wa upinzani nchini Tanzania
hakiwezi kuzima taa ya madai kwa ajili ya demokrasia ya kweli nchini
humo. Viongozi hao wa chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA), walipelekwa jela siku ya Jumanne baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka manane yakiwamo ya
kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT,
Akwilina Akwiline, uasi, kuhamasisha chuki kati ya wanajamii na
kuchochea ghasia nchini Tanzania.
Hayo
yanajiri katika hali ambayo siku chache zilizopita, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe aliviambia vyombo vya habari kwa kuzituhumu asasi
za serikali ya Dar es Salaam ikiwemo polisi kwamba, zilikuwa zinapanga
mkakati wa kuwafungulia kesi ya mauaji na uhaini baadhi ya viongozi wa
chama chake. Kwa mujibu wa Mbowe, lengo
la kutekelezwa mkakati huo ni kuhakikisha kuwa viongozi hao wanawekwa
mahabusu kwa muda mrefu ili kufifisha na kuua kabisa upinzani nchini.
No comments:
Post a Comment