Kamanda wa jeshi la polisi kanda maalum ya
Dar es Salaam nchini Tanzania, Lazaro Mambosasa, amesema kuwa hadi sasa
bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa
kupigwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),
Akwilina Akwilini.
Hata hivyo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameshangazwa
na taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam
Lazaro Mambosasa kuhusu kutojulikana silaha iliyotumika kumuua Akwilina
na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Nimeitafakari kauli
ya Mambosasa inayohusu tukio la Akwilini kuhusu silaha iliyotumika,
bila shaka kuna dhambi kubwa inapangwa nawasihi Wana CHADEMA kuwa makini
wakati huu kwani si ajabu ukasikia kuwa Ile silaha iliyotumika kumuua
Akwilini imekutwa nyumbani kwa Kiongozi wa CHADEMA” -Lema
Kamanda
wa jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa
alisema jana Ijumaa mbele ya waandishi wa habari bado hawajabaini ni
silaha gani ilitumika katika tukio la mauaji ya Akwilina Akwini, ambaye
kifo chake kimezusha malalamiko makubwa ya asasi mbalimbali na kiraia
nchini Tanzania.
“Bado tunaendelea na upelelezi wa tukio
hili. Hatujajua ile silaha iliyotumika hadi kumpata Akwilina kwa sababu
askari walikuwa wengi siku ile na hakukuwa na ushahidi ni yupi
aliyetenda kosa hilo.“ Amesema Mambosasa. Hii ni katika hali ambayo,
tarehe 18 Februari mwaka huu Kamanda Lazaro Mambosasa alinukuliwa
akisema kuwa, jeshi la polisi linawashikilia askari wake sita na silaha
zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Akwilina Akwilini, aliuawa kwa kupigwa
risasi tarehe 16 Februari mwaka huu, wakati polisi walipokuwa
wakiwatawanya wafuasi wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA)
waliokuwa wanaamdamana kuelekea ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni kushinikiza mawakala wao kupatiwa barua za viapo vyao kwa
ajili ya kusimamia uchaguzi mdogo uliopita wa jimbo hilo.