Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran
amesema kuwa, lengo na shabaha kuu ya Marekani ni kuupindua mfumo wa
Kiislamu nchini Iran kupitia njama za kuushambulia mhimili wa Utawala wa
Fakihi (Wilayatul Faqih) humu nchini.
Ayatullah Ahmad Khatami ameyasema
hayo leo katika hotuba za Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran na kuongeza
kwamba, Marekani inafanya njama za kila namna za kutoa pigo dhidi ya
nafasi ya juu ya Utawala wa Fakihi ambayo uongozi wake umepelekea
kusambaratishwa njama mbalimbali za Marekani hasa katika kueneza makundi
ya kigaidi likiwemo lile la Daesh (ISIS) katika eneo hili na kadhalika
kusambaratisha njama za kuanzishwa Mashariki ya Kati Mpya kwa maslahi ya
Marekani na Israel, na kwamba kusambaratishwa njama hizo kumeharibu
ndoto kubwa ya Washington.
Akizungumzia stratijia mpya ya Marekani
dhidi ya Iran ya Kiislamu amesema, stratijia hiyo inajumuisha
kusambaratisha nishati ya nyuklia, kupunguza uwezo wa kiulinzi na uwezo
wa makombora, kukata uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa
Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon na kwa wanamuqawama wa
Palestina na kadhalika kuzuia upinzani wa Tehran wa kupambana na njama
ya kuanzisha Mashariki ya Kati Mpya. Ayatullah Ahmad Khatami amesisitiza
kwamba, viongozi wote wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran wanapinga vikali
hatua yoyote ya kufanya mazungumzo mapya ya nyuklia au kufanyiwa
marekebisho mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kupunguzwa uwezo wa kiulinzi
wa makombora ya Iran ya Kiislamu na kwamba katika uwanja huo taifa hili
halitoruhusu uingiliaji wowote wa kigeni nchini.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini
Tehran ameashiria kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendeshwa kwa
mujibu wa sheria za Qur'an na katiba iliyosimama juu ya msingi wa
mafundisho ya Kiislamu hivyo, itaendelea kuyaunga mkono makundi ya
muqawama ya Palestina na harakati ya Hizbullah ya nchini Lebanon.
Amefafanua zaidi kwa kusema, stratijia ya Washington katika eneo ni
kuzusha machafuko kwa ajili ya kudhamini usalama wa utawala khabithi wa
Kizayuni na kwamba, hivi sasa Marekani inalihamisha kundi la
ukufurishaji la Daesh na kulipeleka Afghanistan kwa ajili ya kudhamini
malengo yake ya kiuchumi na kisiasa katika eneo hili. Pia ameashiria
jinai za hivi karibuni za utawala wa kidikteta wa Saudia nchini Yemen na
matukio ya nchini Bahrain na kusema kuwa, hivi sasa Mohammad Bin
Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme nchini Saudia ameigeuza nchi hiyo kuwa
kama moja ya majimbo ya Marekani.
No comments:
Post a Comment