Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya
Palestina (Hamas) imelaani uamuzi wa Marekani wa kuhamisha ubalozi wake
kutoka Tel Aviv na kuupeleka katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Msemaji wa Hamas, Abdullatif al
Qanou amesema kuwa hatua ya kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel
Avid hadi Quds inayokaliwa kwa mabavu haiupatii utawala wa Kizayuni
uhalali wowote na wala haiwezi kubadili ukweli wa mambo kuhusu mji wa
Quds.
Msemaji Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, Heather Nauert
amesisitiza kupitia taarifa iliyotolewa na wizara hiyo kwamba ubalozi
mpya wa nchi yake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu utafunguliwa
tarehe 14 Mei mwaka huu katika mji wa Quds (Jerusalem).
Rais Donald Trump wa Marekani tarehe
sita mwezi Disemba mwaka 2017 alitangaza kuwa, Washington imeutambua mji
wa Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel licha
ya suala hilo kupingwa pakubwa kieneo na kimataifa na akasema
Washington imeanza mchakato wa kutekeleza uamuzi huo.
Mji wa Quds ambako kuna Msikiti wa al
Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, ni eneo lisiloweza
kutenganishwa na Palestina na ni miongoni mwa maeneo matatu matakatifu
muhimu zaidi kwa Kiislamu. Kwa msingi huo uamuzi wa kifedhuli na kinyume
cha sheria wa Rais wa Marekani wa kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo huko
Baitul Muqaddas ni sehemu ya njama kubwa za Wazayuni na viongozi wa
Marekani dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Chanzo na sababu za uamuzi huo uliodhidi
ya Palestina na dhidi ya Uislamu wa Trump zinapaswa kutathminiwa katika
mitazamo na itikadi zake kama mfuasi au muungaji mkoni wa Wakristo wa
Kizayuni. Tangu aingine madarakani, Trump amekuwa akichukua hatua na
maamuzi ya kichochezi na vitisho kuhusiana migogoro ya kimataifa na ya
kikanda ikiwemo migogoro inayojiri katika eneo la Mashariki ya Kati; na
mgogoro wa Palestina umefanywa ajenda kuu katika kalibu ya siasa na
njama zinazofanywa na Marekani. Siasa hizo za kichochezi za Trump
zinaweza kutathminiwa katika kalibu ya siasa jumla za White House katika
eneo la Mashariki ya Kati katika fremu ya kile kinachojulikana
kama "makubaliano ya karne." Fikra za waliowengi na duru za kisiasa
katika eneo la Mashariki ya Kati zinayataja makubaliano hayo ya karne
kuwa ni sehemu ya mipango yenye lengo la kuifuta kadhia nzima ya
Palestina. Ni katika fremu ya mpango huo mpya wa Marekani kuhusiana na
Quds utakaoishirikisha Israel ambapo Rais Donald Trump wa Marekani
tarehe sita mwezi Disemba mwaka jana alitangaza kuwa anautambua mji wa
Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.
Vilevile wachambuzi wa mambo wanasisitiza kuwa, lengo kuu la hatua ya
Trump ya kuutambua utawala wa Kizayuni kuwa dola la Kiyahudi ni kuandaa
mazingira ya kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kupinga suala
la kuunda nchi ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds na kukanyaga
kikamilifu haki za Wapalestina. Katika mazingira kama hayo, Trump
anafanya kila awezalo ili kuifuta kabisa kadhia ya Quds kwa kusaidiwa na
kuungwa mkono na baadhi ya tawala za Kiarabu katika eneo hili.
Gazeti la al Hayat linalochapishwa London limeandika kuwa:
Israel inataka kunufaika na uamuzi wa Marekani wa kuhamishia ubalozi
wake katika mji wa Quds ili kutekeleza njama ya kuufanya mji huo kuwa wa
Kiyahudi. Gazeti hilo limenukuu mwandishi wa Kipalestina Nabil al Sahli akisema kwamba:
Hatua za kuuhamishia ubalozi wa Marekani huko Quds inatekelezwa kwa
kasi kubwa, suala linalodhihirisha taswira hatari ya maamuzi ya Rais
Donald Trump wa Marekani dhidi ya Quds.
Naye Robin Wright mwandishi habari wa Kimarekani ameandika katika gazeti la New York kuwa: Hatua
ya Donald Trump ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda
Quds itazidisha mgogoro katika Mashariki ya Kati.
Hatua zote hizo za Trump hazitakuwa na
natija nyingine ghairi ya kuimarisha Intifadha ya Tatu ya Wapalestina
ambayo ilianza kujibu maamuzi ya Trump kuhusu Quds. Kwa kuzingatia hisia
walizonazo Wapalestina na Ulimwengu wa Kiislamu na fikra za waliowengi
duniani kwa ujumla kuhusu suala la Quds, hatua yoyote ile ya Marekani ya
kuunga mkono na kuzibariki siasa za kiistikbari za Israel kuhusiana na
Baitul Muqaddas inaweza kuigharimu Marekani kisiasa, kidiplomasia na
kiuchumi.
No comments:
Post a Comment