Marubani wawili wamefariki dunia katika ajali
ya ndege ndogo iliyotokea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid
Amani Karume visiwani Zanzibar.
Vyombo
vya habari vya Tanzania vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa,
marubani wawili Alfred Mcha (26) na Dominic Bomani (64) wamefikwa na
mauti hayo baada ya ndege waliyokuwa wanaifanyia majaribio kuanguka na
kuteketea kwa moto. Habari ya kuanguka na kuteketea kwa moto ndege hiyo
imethibitishwa pia na mhandisi mkuu wa kampuni ya Tropical Air, David
Kisusi.
Ndege hiyo 5H-TDF yenye uwezo wa kubeba
abiria wanne ilikuwa ni mali ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Tanzania
(NIT) na kwamba ilikuweko Zanzibar kwa ajili ya matengenezo.
Kwa mujibu wa David Kisusi, ndege hiyo
ilikuwa uwanjani hapo kwa takriban miezi sita ikifanyiwa matengenezo.
Habari za kidaktari zinasema kuwa, vifo vya marubani hao vilisababishwa
na kukosa hewa safi wakati wa ajali na kuathiriwa na moto mkali.
No comments:
Post a Comment