Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limepasisha azimio la kusitishwa vita kwa siku 30 nchini Syria na
kuruhusu upelekaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo
yanayozingirwa.
Azimio hilo ambalo limepasishwa na wanachama wote 15 wa Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa limeyaondoa makundi ya kigaidi chini ya
mwavuli wa uamuzi huo wa kimataifa kutokana na msimamo imara wa Russia.
Kwa mujibu wa azimio hilo, misaada ya kibinadamu itaanza kutumwa mara
moja katika maeneo yote yanayozingirwa nchini Syria hususan eneo la
Ghouta Mashariki. Eneo hilo la kistratijia lililoko karibu na mji mkuu
wa Syria, Damascus, linadhibitiwa na makundi ya kigaidi yanayoungwa
mkono na Marekani, Saudi Arabia na washirika wao, na serikali ya Rais
Bashar Assad inafanya jitihada za kulikomboa na kuwafurusha magaidi
katika eneo hilo.
Magaidi hao wamekuwa wakitumia eneo hilo la Ghuota Mashariki
kushambulia mji mkuu wa Syria kwa maroketi karibu kila siku na kuua raia
wasio na hatia.
Baada ya kupasishwa azimio hilo balozi na mwakilishi wa Russia katika
Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzya amekosoa sera za kibeberu za muungano
unaoongozwa na Marekani huko Syria na kusema, makundi ya waasi
yanayosaidiwa na muungano huo ndiyo yanayohusika na mgogoro wa
kibinadamu katika eneo la Ghuota Mashariki.
Nebenzya
pia amekosoa propaganda chafu zinazofanywa na vyombo vya habari vya
nchi za Magharibi dhidi ya majeshi ya serikali ya Syria katika mapigano
ya sasa huko Ghuota Mashariki.
No comments:
Post a Comment