Saturday, February 24, 2018

KIGOGO WA MAKASINO KUGHARAMIA KUHAMISHIWA UBALOZI WA MAREKANI BAITUL-MUQADDAS

Kigogo wa makasino kugharamia kuhamishiwa ubalozi wa Marekani Baitul-Muqaddas
Sheldon Adelson, bilionea wa Kiyahudi ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa utawala ghasibu wa Israel ametangaza kuwa, atatoa gharama za kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baitul-Muqaddas.
Sheldon Adelson ambaye anatambulika kama kigogo wa makasino kutokana na kumiliki vilabu vingi vya anasa amesema kuwa, atatoa sehemu ya gharama za kuhamishiwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Baitul-Muqaddas.
Bilionea huyo ambaye alitoa dola milioni tano kwa ajili ya hafla ya kuapishwa Donald Trump anahesabiwa kuwa muungaji mkono mkubwa wa kifedha wa chama cha Republicans na mtu anayemkingia kifua na kumuunga mkono kwa kila hali Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel.
Sheldon Adelson anahesabiwa kuwa miongoni mwa watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Iran ambaye amewahi kumpendekezea Rais Donald Trump aishambulie Iran kwa mabomu ya atomiki.
Rais Donald Trump wa Marekani
Myahudi huyo mwenye chuki na Wapalestina ametangaza nia yake ya kutoa sehemu ya gharama za kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Beitul Muuqaddas baada ya hivi karibuni kutangazwa kuwa, Washington imeazimia kuuhamishia ubalozi wake mjini humo mwezi Mei mwaka huu.
Tarehe 6  Disemba mwaka jana, Rais wa Marekani aliitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na akatoa amri ya kufanyika taratibu za kuuhamishia mjini humo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala dhalimu wa Kizayuni.

No comments:

Post a Comment