Maelfu ya raia wa Burundi Jumamosi ya jana
waliandama mjini Bujumbura, katika kulalamikia ripoti ya hivi karibuni
ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inayopinga suala la kufanyiwa
marekebisho katiba ya nchi hiyo ili kumruhusu Rais Pierre Nkurunziza
kugombea katika uchaguzi ujao.
Katika maandamano hayo, Warundi
walibeba mabango yaliyokuwa na jumbe za kumtuhumu Michel Kafando, mjumbe
maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwamba anatumikia maslahi ya
baadhi ya nchi za Ulaya hususan Ubelgiji, mkoloni wa zamani wa Burundi.
Kadhalika waandamanaji wamekosoa msimamo
wa António Guterres na kuutaja kuwa unaoingilia masuala ya ndani ya
Burundi. Hivi karibuni António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
alitoa taarifa mbele ya wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la umoja huo
akikosoa sisitizo la viongozi wa Burundi kwa ajili ya kuifanyia
marekebisho katiba ya nchi hiyo bila kuzingatia maoni ya wapinzani.
Katika ripoti hiyo Guterres aliashiria kwamba, juhudi za serikali ya
Bujumbura kwa ajili ya kuifanyia marekebisho katiba, zitapelekea
kuchochea mzozo kati yake na wapinzani. Ikiwa kura ya maoni itafanyika
na kufanyiwa marekebisho ya katiba, basi Rais Pierre Nkurunziza atakuwa
na uwezekano wa kusalia zaidi madarakani hadi mwaka 2030.
Hii ni katika hali ambayo Jumatano
iliyopita kulianza zoezi la uorodheshaji majina ya wapiga kura katika
daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki
katika kura ya maoni. Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwezi
April mwaka 2015 baada ya Rais Nkurunziza kutangaza azma yake ya
kugombea katika uchaguzi wa rais uliopita, ambapo wapinzani waliitaja
hatua hiyo kuwa ni kukiuka katiba huku kwa upande wake serikali ya
Bujumbura ikisema kuwa bado rais huyo hajakiuka katiba.
No comments:
Post a Comment