Wakaguzi wa umoja wa Mataifa wanasema zaidi
ya maafisa 40 wa Jeshi la Sudan Kusini wanaaminika kutenda jinai za
kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Wakaguzi
hao wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini
wamesema msingi wa uchunguzi wao ni mahojiano waliyofanya na mamia ya
mashuhuda, picha za satalaiti na nyaraka 60,000 tokea vita vianze nchini
humo mwaka 2013.
Ripoti hiyo
ambayo ilichapishwa Ijumaa inasema maafisa wa ngazi za juu jeshini
wamehusika na hujuma za makusudi dhidi ya raia. Kati ya wanoatuhumiwa ni
maluteni jenerali wanane na magavana wa majimbo matatu.
Hii ni mara
ya kwanza kwa ripoti za Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan Kusini kuwataja
wahusika wa jinai kinyume na miaka ya nyuma ambapo ripoti hizo zilikuwa
zikitaja tu jinai zilizotendwa.
Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini Mawien Makol amesema serikali ya nchi hiyo iko tayari kumshtaki yeyote aliyehusika na jinai.
Hayo
yanajiri wakati ambao Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametamka bayana
kwamba Marekani ndiyo ambayo inasababisha ukosefu wa amani ndani ya nchi
yake changa zaidi barani Afrika.
Rais Kiir aliyasema hayo Ijumaa katika mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mjini Kampala Uganda.
Vita vya
ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya
maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi
hiyo, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya
ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu
wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na
jaribio la kupindua serikali yake.
No comments:
Post a Comment