Boris Johnson, waziri wa mambo ya nje wa
Uingereza Ijumaa alianza safari ya kuzitembelea nchi tatu mashariki mwa
Asia za Bangladesh, Myanmar na Thailand.
Akiwa nchini Bangladesh, Johnson
alitembelea pia kambi moja ya wakimbizi ya Waislamu wa jamii ya
Rohingya. Moja ya ajenda kuu za mazungumzo ya waziri huyo wa mambo ya
nje wa Uingereza na viongozi wa Bangladesh ilikuwa ni hali ya kutisha
mno ya Waislamu wa Myanmar. Kabla ya kuanza safari yake ya kuzitembelea
nchi hizo tatu, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza alisema kuwa, msiba
mkubwa na maafa yaliyowakumba Waislamu wa jamii ya Rohingya, ni moja ya
majanga ya kutisha zaidi duniani katika zama hizi. Johnson si kiongozi
wa kwanza na hatokuwa wa mwisho wa nchi za Magharibi kuzungumzia hali
mbaya sana ya Waislamu wa Myanmar.Miezi michache iliyopita pia, viongozi wengine wa nchi za Magharibi walielezea kusikitishwa kwao na majanga waliyobebeshwa Waislamu wa jamii ya Rohingya na kufikia hata kutembelea kambi za wakimbizi za Waislamu hao huko Banghladesh. Aghlabu ya viongozi hao wa nchi za Magharibi walielekea pia nchini Myanmar na kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo. Lakini wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, yote hayo yanafanyika kwa malengo ya kipropaganda na kujitoa kimasomaso mbele ya walimwengu, kwani hadi hivi sasa safari na matamshi ya viongozi hao wa Magharibi hayajasaidia chochote zaidi ya kuzidi kuteseka tu Waislamu wa Myanmar ambao kwa ungamo la Umoja wa Mataifa, ni jamii ya wachache inayodhulumiwa zaidi ulimwenguni.
Jeshi la Myanmar na mabudha wenye misimamo mikali wamefanya na wanaendelea kufanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Hadi sasa wameshaua mamia ya Waislamu na kuwanajisi maelfu ya wasichana na wanawake wa jamii hiyo. Jinai za mtawalia za jeshi la Myanmar zimewalazimisha Waislamu laki saba wa jamii ya Rohinghya kukimbilia Bangladesha na hivi sasa wanaishi katika mazingira magumu mno kwenye kambi za wakimbizi. Hata hivyo tawala za nchi za Magharibi zinatosheka tu na kuitaka kwa maneno serikali ya Mynamar kuheshimu haki za Waislamu wao. Serikali ya Myanmar inaendelea kufanya kiburi na kudai kuwa eti Waislamu nchini humo hawabaguliwi na eti hakuna jinai yoyote wanayofanyiwa.
Aung San Suu Kyi ambaye hivi sasa ni kiongozi nambari moja wa Myanmar alipitisha muda mwingi jela pamoja na kifungo cha nyumbani wakati alipokuwa anaendesha mapambano dhidi ya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo. Wamagharibi walimpa tunzo ya amani ya Nobel kutokana na mapambano yake hayo. Madaraka ya Myanmar hivi sasa yako mikononi mwa bibi huyo na wale wale wanajeshi waliomfunga jela miaka mingi, ndio hao hao ambao hivi sasa wanafanya jinai kubwa mno ya kuangamiza kizazi cha Waislamu. Sasa badala ya Aung San Suu Kyi kukumbuka mateso aliyofanyiwa na wanajeshi hao wakati wa mapambano yake, amegeuka kwa daraja 180 na kuunga mkono jinai zao huku akikanusha kabisa kuwa hakuna jinai bali hata ubaguzi wanaofanyiwa Waislamu nchini Myanmar. Si hayo tu, lakini pia serikali ya Aung San Suu Kyi imefunga milango yote ya kuingia na kutoka maeneo ya Waislamu hao ili kuzuia walimengu wasione upeo wa kupindukia wa jinai wanazofanywa Waislamu hasa katika jimbo la Rakhine, la magharibi mwa Myanmar.
Bi Yanghee Lee, ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar ametangaza habari ya kuendelea ukandamizaji na uvunjaji wa haki za binadamu nchini humo. Amesema, licha ya kuweko serikali ya kiraia inayoongozwa na Aung San Suu Kyi, lakini baadhi ya vitendo vya serikali hiyo ni vya ukandamizaji na ni sawa na vile vile vilivyokuwa vikifanywa na serikali ya wanajeshi.
Kwa kweli ni kwa muktadha huo ndio maana weledi wa mambo wakasema kuwa, matamshi na ziara za mara kwa mara za viongozi wa nchi za Magharibi zinazoonekana kama ni za kufuatilia jinai za wanajeshi wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya si lolote si chochote ghairi za siasa za kipropaganda tu zisizo na manufaa yoyote kwa Waislamu hao.
No comments:
Post a Comment