Friday, February 23, 2018

MIILI YA VIJANA WATATU WA BAHRAIN WALIOULIWA NA UTAWALA WA AAL KHALIFA, YAZIKWA MJINI QUM, IRAN

Miili ya vijana watatu wa Bahrain waliouliwa na utawala wa Aal Khalifa, yazikwa mjini Qum, Iran
Miili ya vijana watatu wa mapinduzi ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa na waliouliwa na polisi wa utawala huo, walizikwa jana Ijumaa mjini Qum, kusini mwa Tehran.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, wiki iliyopita polisi wa utawala wa Bahrain uliwaua kidhulma vijana wanne wa nchi hiyo, na katika kujaribu kuficha jinai hiyo waliitupa miili ya mashahidi hao baharini. Miili mitatu ya vijana hao iliokotwa katika pwani ya mkoa wa Bushehr, kusini mwa Iran. Watu hao waliouawa ni Sayyid Qasim Khalil Darwish, Maitham Ali Ibrahim, Sayyid Mahmud na Sayyid Adel Kadhim.
Hamad bin Isa Al Khalifa, Mfalme wa Bahrain akiwa na Rais Trump wa Marekani
Katika mazishi yao ambayo yalihudhuriwa na watu wengi kutoka matabaka tofauti, washiriki walibeba picha za Ayatullah Sheikh Isa Qassim, alimu mkubwa wa Bahrain ambaye maisha yake yako hatarini kutokana na njama za utawala huo, kama ambavyo pia walibeba picha za baadhi ya mashahidi waliouawa tangu zilipoanza harakati za mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 nchini Bahrain. Kadhalika washiriki walipiga nara za mauti kwa Marekani na mauti kwa Israel sambamba na kulaani kimya cha jamii ya kimataifa kutokana na jinai za kila leo zinazofanywa dhidi ya raia madhlumu wa Bahrain.
Askari wa Saudia na Bahrain hawajawaonea huruma hata wanawake
Harakati ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kidikteta wa nchi hiyo ilianza tarehe 14 Februari mwaka 2011 ambapo raia hao walikuwa wakilalamikia kukosekana uadilifuu, uhuru, kuweko ubaguzi na kutaka marekebisho ya kisiasa nchini humo. Hata hivyo ukoo wa kifalme wa Aal Khalifa badala ya kusikiliza kilio hicho cha wananchi uliomba msaada wa maelfu ya askari wa Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu na kufanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya raia wake. Kama hiyo haitoshi utawala huo wa kiimla unaendelea kutekeleza siasa kandamizi ikiwa ni pamoja na mauaji dhidi ya raia, kuwafunga jela, kuwanyonga, kuwahukumu vifungo vya maisha na mambo mengi kama hayo.

No comments:

Post a Comment