Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran amebainisha misimamo ya Tehran kuhusiana na matukio ya kieneo na
kimataifa katika mkutano wake na waandishi wa habari wa ndani na wa nje
na kusema kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwamba, katu
hakutoongezwa au kupunguzwa chochote katika makubaliano hayo.
Akijubu swali kwamba, Rais Donald
Trump amekuwa akisisitiza kuwa, kama makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
hayatafanyiwa marekebisho, Marekani itaanza tena kuiwekea vikwazo Iran
na kwamba, Washington itajitoa katika makubaliano hayo, je katika
mazingira haya Ira itachukua uamuzi gani? Rais Rouhani amesema kuwa,
Iran haitakuwa ya kwanza kukiuka makubaliano ya nyuklia na hakuna
kitakachoongezwa au kupunguzwa katika makubaliano hayo.
Rais Rouhani amesisitiza kwamba, Iran
itaendelea kubakia na kufungamana na makubaliano ya nyuklia madhali kuna
maslahi na manufaa na kwamba, uamuzi wa Marekani wa kubakia au kujitoa
katika makubaliano hautakuwa na taathira yoyote kwa uamuzi wa Jamhuri ya
Kiislamu. Kuhusiana na kung'ang'ania Marekani kufanyika mazungumzo
mapya kuhusiana na baadhi ya mambo katika makubaliano ya nyuklia na
kudhibitiwa mpango wa makombora wa Iran, Rais Hassan Rouhani amesisitiza
kwamba, Iran haifuatilii suala la kuwa na silaha za maangamizi
ya umati na haribifu kama inavyofanya Marekani na baadhi ya nchi, lakini
kuhusiana na silaha za kawaida, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
itatengeneza na kumiliki silaha hizo kwa kadiri ya mahitahi ya kiulinzi
na kujihami na kwamba, haitafanya mazunguumzo na yeyote kuhusiana na
suala hilo.
Januari 12 mwaka huu, Rais wa Marekani aliongeza kwa mara ya tatu
muda wa kusimamishwa vikwazo dhidi ya Iran lakini akatangaza masharti ya
kubakia nchi yake katika makubaliano ya nyuklia kama vile kubadilishwa
baadhi ya vipengee vya makubaliano hayo, kuruhusu kukaguliwa vituo vya
kijeshi vya Iran na kudhoofishwa mpango wa makombora wa Tehran na
akasema pia kwamba, endapo Kongresi na Ulaya hazitatekeleza masharti
hayo, wakati ujao hataongeza muda wa kusimamishwa vikwazo dhidi ya Iran
na nchi yake itajitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa
Rais nchini Marekani Donald Trump alitangaza bayana chuki na uadui wake
dhidi ya makubaliano ya JCPOA na akasisitiza kwamba, kama atachaguliwa
kuwa Rais wa nchi hiyo atayachana makubaliano hayo. Katika radiamali
yake kwa msimamo huo wa Trump, Iran ilitoa onyo kali na kusisitiza
kwamba, endapo Trump atayachana makubaliano hayo basi Iran itayachoma
moto. Msimamo thabiti na imara wa Iran mbele ya serikali ya sasa ya
Marekani umemchanganya Trump na washauri wake na hii leo licha ya kupita
mwaka mmoja tangu Trump ashike hatamu za uongozi wa White hajaweza
kuleta mabadiliko katika makubaliano hayo ya nyuklia.
Juhudi zote za Trump ni kuhakikisha kwamba, kupitia makubaliano ya
JCPOA na uropokaji wake aweze kuleta mabadiliko katika siasa za kigeni
za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Mashariki ya Kati ambapo wenzo huu
wa Trump hauwezi kusaidia chochote na wala hauwezi kurejesha nyuma hali
ya hivi sasa. Iran ni dola lenye nguvu katika Mashariki ya Kati na
imekuwa na taathira katika mahesabu ya eneo na bila shaka makelele
kuhusu JCPOA na njama za kutishia uwezo wa makombora ya Iran ni mambo
ambayo kwa hakika hayawezi kumfanya Trump na waungaji mkono wake kama
Saudia na Israel kufikia malengo yao.
Nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu katika
eneo ni nafasi ambayo haiwezi kuathiriwa na mambo yasiyo na maana ya
lobi za Wazayuni au domokaya na makelele ya Trump. Nguvu ya Iran katika
Mashariki ya Kati chimbuko lake ni uungaji mkono wa wananchi na
kutegemea mamlaka yake ya kujitawala na nguvu hii imekuwa na taathira
pia kwa eneo hili.
No comments:
Post a Comment