Saturday, February 3, 2018

TRUMP NA UNGAMO LA UDHAIFU WA JESHI LA MAREKANI

Trump na ungamo la udhaifu wa jeshi la Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump ameungama na kukiri hadharani kuwa jeshi la nchi hiyo ni dhaifu na ametaka wizara ya ulinzi, Pentagon, itengewe fedha nyingi zaidi.
Trump amekiri hayo mbele ya kadamnasi ya viongozi wa chama chake cha Republican na kusisitiza kuwa, jeshi la Marekani ni dhaifu kwa muda mrefu tu hata kabla ya kuingia madarakani Barack Obama. Amesema, kuna wajibu wa kulijenga upya jeshi la Marekani na kuongeza kuwa: Tunahitajia kuwa na jeshi kubwa lenye nguvu. Tunapaswa tuwe na nguvu kubwa zaidi ya tulizokuwa nazo huko nyuma.
Matamshi hayo ya Trump yametolewa kwenye hali ambayo katika mwaka wa hivi sasa wa fedha, Marekani imetenga dola bilioni 700 kwa ajili ya wizara yake ya ulinzi Pentagon; kiwango kikubwa sana cha fedha ambacho hakijawahi kutengewa wizara hiyo katika miongo mingi iliyopita. Inatabiriwa kuwa kiwango cha bajeti ya wizara hiyo ya ulinzi ya Marekani kitaongezewa dola zisizopungua bilioni 20 juu ya bajeti yake ya hivi sasa katika makadirio ya mwaka ujao wa fedha. Kwa maneno mengine ni kuwa, bajeti ya ulinzi ya Marekani katika kipindi cha miaka miwili kitakuwa ni takriban dola trilioni moja na nusu; fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya kukarabati miundombinu iliyochakaa ya Marekani. Ikumbukwe kuwa, bajeti ya ulinzi ya Marekani inakadiriwa kuwa sawa na nusu ya bajeti zote wa ulinzi za nchi nyingine duniani.
Jeshi la Marekani nchini Syria
 
Pamoja na kutengwa fedha hizo nyingi, lakini rais wa Marekani amejitokeza mbele ya kadamnasi ya watu na kuungama kuwa jeshi la nchi hiyo linazidi kuwa dhaifu. Hata hivyo, udhaifu huo hautokani na kukosekana silaha za kisasa zenye uwezo wa kufanya uharibifu mkubwa, hapana, bali udhaifu wa jeshi la Marekani unatokana na kupoteza nguvu zake katika vita laini sambamba na kuzidi kuongezeka uwezo wa kiulinzi wa nchi zinazoipinga Marekani. Tajiriba iliyopatikana katika vita vya Iraq inaonesha kuwa, jeshi la Marekani lilitumia takriban siku 20 tu na kupoteza wanajeshi 140 katika kampeni ya kuupindua utawala wa Baath wa Saddam Hussein. Hata hivyo ilishindwa kurudisha utulivu nchini humo licha ya kupita miaka mingi ya kuikalia kwa mabavu Iraq kama ambavyo imepoteza zaidi ya wanajeshi 4,300 huko Iraq pekee katika kipindi hicho. Hali ni hivyo hivyo katika nchi jirani na Iraq yaani Syria. Licha ya Marekani kutumia fedha nyingi na silaha za kila namna kuyaunga mkono magenge ya kigaidi yaliyokuwa yanafanya jinai ndani ya ardhi ya Syria, lakini muungano wa Magharibi na baadhi ya Waarabu unaoongozwa na Marekani umefeli vibaya huko Syria. Hata jinai ya Marekani ya kuvurumisha zaidi ya makombora 50 dhidi ya wanajeshi wa Syria nayo haikusaidia Marekani na vibaraka wake. Kufeli jeshi la Marekani hakumalizikii Syria na Iraq tu, bali udhaifu wa jeshi hilo lenye majigambo na majivuno mengi umeonekana pia mashariki mwa bara la Asia. Korea Kaskazini imepuuza kikamilifu makeke ya Marekani na kuendelea kujiimarisha kwa makombora na silaha za nyuklia na hivi sasa ardhi ya Marekani iko katika hatari ya kushambuliwa kwa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini.
Hubert VĂ©drine, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa
 
Hubert VĂ©drine, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa anasema: zama za kambi moja ya Marekani zimemalizika kwa manufaa ya madola mengine yenye nguvu. 
Hivi sasa viongozi wa Marekani na hususan wenye misimamo mikali na chuki dhidi ya wageni kama vile Donald Trump wanahaha na wanatafuta kila njia ya kuondoa udhaifu wa jeshi hilo kwa kutumia matrilioni ya dola za walipa kodi huko Marekani. Hata hivyo kasi ya mabadiliko katika karne hii ya 21 ni kubwa, madola mapya yenye nguvu kimataifa yanazidi kujitokeza na hii haina maana nyingine isipokuwa kuzidi Marekani kupoteza taathira na ushawishi wake katika mfumo wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment