Jeshi la Yemen likishirikiana na wapiganaji
wa Harakati ya Ansarullah wamevurumisha kombora la balisitiki ndani ya
ardhi ya Saudi Arabia na kulenga kituo cha kijeshi katika eneo la Jizan.
Taarifa zinasema kombora ambalo limetumika katika oparesheni
hiyo ni Qaher M-2 ambalo limetengenezwa ndani ya Yemen. Shirika la
Habari la Yemen, Saba, limesema kombora hilo limesababisha hasara kubwa
katika kituo hicho cha jeshi la Saudia.
Jumamosi pia Kitengo cha Makombora cha Harakati ya Ansarullah ya
Yemen kilitangaza kuwa kimevurumisha kwa mafanikio kombora la balistiki
ambalo limelenga kituo cha Jeshi la Saudia katika mkoa wa Najran kusini
mwa ufalme huo.
Halikadhalika Ijumaa Harakati ya Ansarullah ilitangaza kuwa ililenga
kwa mafanikio kituo cha mafuta cha kampuni ya Aramco ya Saudia katika
mkoa wa Jizan. Kombora lililotumika katika iparesheni hiyo pia nia
Badr-1. Aidha Jumatatu liyopita wapiganaji wa Ansarullah wakishirikiana
na Jeshi la Yemen walishambulia kwa makombora ya balistiki uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid katika mji wa Riyadh mji mkuu wa
Saudia, uwanja wa ndege wa Abha huko Asir na uwanja wa ndege wa Jizan
unaopatikana kusini mwa Saudi Arabia.
Mashambulizi hayo yote ni katika oparesheni za kulipiza kisasi jinai
za Saudia dhidi ya raia wa Yemen. Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha
hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la
kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi
aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh.
Raia zaidi ya elfu 14 wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na
maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi. Aidha watu
karibu milioni moja wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote nchini
Yemen huku wengine karibu 3,000 wakifariki dunia tokea mwezi Aprili
mwaka jana. Mamilioni ya Wayemen pia wamepoteza makazi yao kutokana na
hujuma hizo za Saudia.
No comments:
Post a Comment