Tuesday, April 17, 2018

MAHAKIMU ZAIDI YA 250 WAFUTWA KAZI JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO

Mahakimu zaidi ya 250 wafutwa kazi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewafuta kazi zaidi ya mahakimu 250 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya ufisadi.
Waziri wa Sheria Alexis Thambwe Mwamba amesema kuwa, mahakimu hao wamefutwa kazi kwa sababu za ufisadi na wengine kutokuwa na elimu ya taaluma hiyo.
Waziri thambwe amebainisha kuwa, hatua hii imechukuliwa ili kuwazuia watu waliokuwa wakiingia katika idara ya mahakama wakiwa na lengo la kujipatia fedha badala ya kuwatumikia raia wa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, idadi kamili ya mahakimu waliofutwa kazi na serikali ni 256 na kwamba, sababu kuu ni majaji hao kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, kutokuwa na elimu ya taaluma hiyo na kundi la tatu limestaafishwa.
Alexis Thambwe Mwamba, Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Kinshasa kuwachukulia hatua maafisa wa juu wa idara ya Mahakama. Mwaka 2009, Rais Joseph Kabila aliwafuta kazi majaji 96 baada ya kubainika kuwa walikuwa wakijihusha na vitendo vya ufisadi.
Hatua hiyo ya kufutwa kazi majaji hao inakuja kukiwa kumesalia miezi 7 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu katika nchi hiyo inayokabiliwa na changamoto kubwa ya usalama. 
Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka jana ulisogezwa mbele na sasa unatarajiwa kufanyika Desemba 23, mwaka huu ili kumpata mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye muhula wake wa uongozi ulimalizika Desemba 20, 2016.

Friday, April 13, 2018

MAGAIDI WA BOKO HARAM WAMEWATEKA WATOTO ZAIDI YA 1,000 TOKEA 2013

Magaidi wa Boko Haram wamewateka watoto zaidi ya 1,000 tokea 2013
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria wamewateka watoto zaidi ya 1,000 tokea mwaka 2013.
Hayo yamedokezwa katika ripoti mpya ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto, UNICEF ambayo imetolewa kwa munasaba wa kutekwa wasichana 276 wa shule katika mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria. Wasichana hao walitekwa na magaidi wa kundi hilo la Kiwahhabi la Boko Haram.
Mkuu wa UNICEF nchini Nigeria Mohamed Malick Fall amesema watoto katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi ambayo yanashtua sana. UNICEF imesajili kesi zaidi ya 1,000 za watoto kutekwa nyara lakini imesema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi. Aidha shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema limemhoji msichana aliyewahi kutekwa na Boko Haram ambaye sasa ana umri wa miaka 17 ambaye amesema alinajisiwa na wapiganaji wa kundi hilo. Anasema alipata mimba baada ya tukio hilo la kusikitisha na sasa anakabiliwa na matatizo mengi katika kambi ya wakimbizi huku akikejeliwa kuwa  yeye ni 'mke wa wapiganaji wa Boko Haram'.
Katika usiku wa Aprili 14 kuamkia 15, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara wasichana 276 ambao wengi wameshaachiliwa lakini 100 bado hawajulikani waliko na kuna wasi wasi kuwa baadhi wameshafariki huku baadhi wakiwa wameamua kubakia huko walikotekwa nyara.
UNICEF inasema tokea uanze uasi wa magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria, hadi sasa waalimu zaidi ya 2,295 wameuawa na shule 1,400 kubomolewa.
Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.
Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.

DRC YASUSIA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA WA KUKUSANYA FEDHA ZA KUWASAIDIA RAIA WA NCHI HIYO

 DRC yasusia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kukusanya fedha za kuwasaidia raia wa nchi hiyo
Mkutano maalumu uliotishwa na Umoja wa Mataifa umeanza leo mjini Geneva Uswisi kwa kuchangisha fedha za kukabiliana na janga la kibinaadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo huku serikali ya Kinshasa ikiususia mkutano huo.
Mashirika ya misaada yanasema kuwa, zaidi ya watu milioni 5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia yya Congo kwa sababu ya mapigano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Aidha mkutano huo  wa wafadhili umeanza leo huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionesha kwamba, watu milioni 13 wanahitaji msaada huku thuluthi moja kati yao wakiwa  ni wakimbizi wa ndani  ambao wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu mwaka huu.
Wafadhili hao wa kimataifa wanatafuta  kiasi cha dola bilioni 1.7 kuwasaidia watu hao wanaohitaji dawa, chakula na makazi mazuri.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesusia mkutano huo, ikiyashutumu mashirika ya kiraia kwa kutoa takwimu za uongo na kulichafulia jina taifa hilo.
Uamuzi huo wa serikali ya Kinshasa wa kususia mkutano huo umekosolewa, huku baadhi ya wakosoaji wakisema kwamba, serikali yya Kinshasa ingeshiriki tu katika mkutano huo ili kuwashajiisha wafadhili watoe misaada kwani wanaoumia ni raia.
Hayo yanajiri katika hali ya ambayo, hivi karibuni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  lilionya kuwa, hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kuwa mbaya na imefikia hatua ya kuwa janga kwenye baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na njaa.

AYATULLAH AKHTARI: MAWAHABI WANAPIGWA NA WANAZUONI NA MATAIFA YA KIISLAMU

Ayatullah Akhtari: Mawahabi wanapingwa na wanazuoni na mataifa ya Kiislamu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimatataifa ya Ahlul-Beit (AS) amesisitiza kuwa, utawala wa Aal Saud hauna nafasi yoyote si ya kielimu wala uungaji mkono wa wananchi na kwamba, akthari ya wanazuoni wa Kiislamu wanawapinga Mawahabi wa Saudi Arabia.
Ayatullah Muhammad Hassan Akhtari amesema hayo akiwa nchini Syria na kubainisha kwamba, Maulama waliowengi wa Kiislamu na mataifa ya Kiislamu wanachukia Uwahabi ulioletwa na Aal Saud.
Ayatullah Akhtari ameongeza kuwa, aidiolojia ya uchupaji mipaka ya Uwahabi ambayo inaenezwa na kuungwa mkono na Saudi Arabia imepelekea kutokea magaidi ambao wamekuwa wakifanya mashambulio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Katibu Mkuu wa Jumuiya yay Kimataifa ya Ahlul-Beit (AS) amesema Saudia inataka kulinda nafasi yake kupitia kuzusha hitilafu na mifarakano pamoja na kutekeleza mauaji dhidi ya raia wasio na hatia.
Uwahabi
Aidha ameashiria juhudi za utawala wa Saudi Arabia za kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusema kuwa, hatua hiyo ya utawala wa Riyadh inalenga kuulinda na kuuhifadhi utawala huo, hata hivyo jambo hilo linalaaniwa na Waislamu ulimwenguni.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Jumuiya yay Kimataifa ya Ahlul-Beit (AS) amesema kuwa, Saudia imeamua kuuunga mkono utawala dhalimu wa Israel ili kuifurahisha Marekani.
Ayatullah Akhtari ameashiria pia kwamba, watawala wa Saudia wamebomoa athari nyingi za Kiislamu katika miji mitakatifu ya Makka na Madina na kuongeza kwamba, wanachofuatilia Aal Saud ni kuzusha fitina na mifarakano miongoni mwa Waislamu.

Thursday, April 12, 2018

WANARIADHA 13 WA AFRIKA ' WATOWEKA' AUSTRALIA

Wanariadha 13 wa Afrika 'watoweka' Australia
Wanariadha 13 wa Afrika walioenda kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia wametoweka katika mazingira ya kutatanisha.
David Grevemberg, Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola amewaambia waandishi wa habari leo Alkhamisi mjini Gold Coast kunakofanyika mashindano hayo kuwa: "Wanariadha wengine watano raia wa Rwanda, Uganda na Sierra Leone wametoweka na kwenda kusikojulikana."
Ameongeza kuwa, hii ni baada ya wanariadha wengine wanane kutoka Cameroon kutoweka hapo awali, na sasa idadi hiyo ya wanaichezo wa Kiafrika waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha nchini humo imefikia 13.
Serikali ya Australia imetoa viza kwa wanamichezo wanaoshiriki katika michezo hiyo, kuendelea kuwa nchini humo hadi tarehe 15 mwezi Mei. 
Wakimbizi kutoka nchi mbalimbali duniani huko Australia
Peter Dutton, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Australia ameonya kuwa, mwanariadha yeyote atakayebaki nchini humo kinyume cha sheria baada ya muda wake wa viza kumalizika, atafurushwa nchini humo kwa nguvu.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2000 wakati wa mashindano mengine ya Jumuiya ya Madola jijini Sydney, wanaridha zaidi ya 100 waliendelea kuishi katika jiji hilo hata baada ya kumalizika kwa michezo hiyo.

KREMLIN YAJIBU TWITTER YA TRUMP: MAKOMBORA EREVU YANAPASWA KUELEKEZWA KWA MAGAIDI, SI KWA SERIKALI HALALI

Kremlin yajibu Twitter ya Trump: Makombora erevu yanapaswa kuelekezwa kwa magaidi, si kwa serikali halali
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin amesema Moscow Russia haishiriki katika udiplomasia wa Twitter.
Dimitri Peskov ameyasema hayo akijibu ujumbe ulioandikwa na Rais Donald Trump wa Marekani katika mtandao wa kijamii wa Twitter ambaye ameitahadharisha Russia kwamba isubiri makombora ya Marekani huko Syria.  
Peskov amesema kuwa, Russia inaunga mkono hatua madhubuti na inaamini kuwa ni muhimu kujiepusha na hatua yoyote inayoweza kuchafua zaidi hali iliyopo hivi sasa.
Mapema leo Rais Donald Trump wa Marekani aliimbia Russia kupitia mtandao wa Twitter kwamba ijitayarishe kwa mashambulizi ya makombora "mazuri, mapya na erevu" huko Syria. Marekani inadai serikali ya Syria imetumia silaha za gesi ya sumu katika eneo la Douma huko Ghuta Mashariki, suala linalokadhibishwa na Syria na Russia. 
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya kigeni ya Russia, Maria Zakharova pia amejibu matamshi hayo akisema: Mashambulizi erevu yanapaswa kuelekezwa kwa magaidi ni si kwa serikali halali ya Syria.
Image Caption
Russia pia imesema kuwa itayatungua makombora yote ya Marekani yatakayopigwa kueleka Syria na kwamba itapiga mahala yatakakotokea.

Monday, April 9, 2018

ARAB LEAGUE YALAANI JINAI ZA KARIBUNI ZA UTAWALA WA KIZAYUMI DHIDI YA WAPALESTINA

Arab League yalaani jinai za karibuni za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amelaani jinai za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina.
Ahmad Abul Ghait amelaani jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake katika kuwalinda raia wa Palestina mbele ya jinai za utawala wa Israel. 
Ahmad Abul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League
Mahmoud Afifi, msemaji wa Katibu Mkuu wa Arab League pia jana alitahadharisha kuhusu kuendelea jinai hizo za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kueleza kuwa hali ya mambo katika eneo hilo inahitajia uingiliaji wa jamii ya kimataifa. Afifi alisisitiza kuwa wale wote waliohusika na jinai dhidi ya raia wa Palestina huko Ghaza inapasa wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. 
Maelfu ya Wapalestina tarehe 30 mwezi uliopita wa Machi walifanya maandamano ya amani katika maadhimisho ya mwaka wa 42 wa "Siku ya Ardhi" kuelekea katika mpaka wa Ghaza na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; ambapo waandamanaji hao walikabiliwa na hujuma na mashambulizi ya utawala wa Israel. Katika siku hiyo ya maandamano hayo ya amani chini ya anuani ya "Haki ya Kurejea", Wapalestina 17 waliuliwa shahidi na wengine zaidi ya 1400 walijeruhiwa. Tangu siku hiyo hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 29 wameshauliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel na wengine zaidi ya 3000 wamejeruhiwa. Nchi nyingi na vile vile taasisi za kimataifa zimelaani jinai hizo za Wazayuni.

HATIMAYE SPIKA WA BUNGE LA SOMALIA AJIUZURU

Hatimaye Spika wa Bunge la Somalia ajiuzulu
Spika wa Bunge la Federali la Somalia, Mohamed Sheikh Osman Jawari, hatimaye amejiuzulu baada ya nchi hiyo ye Pembe ya Afrika kushuhudia taharuki na mgogoro mkubwa wa kisiasa kwa wiki kadhaa.
Dahir Amin Jesow, mmoja wa wabunge ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Asubuhi ya leo tulikuwa tunajiandaa kujadili hoja ya kumuondoa madarakani Spika, mara ghafla Naibu Spika akaja na barua ya kujiuzulu Spika huyo na kuisoma mbele yetu. Tumepongeza hatua hiyo ya kujiuzulu ambayo inakubalika kikatiba, na tunatumai huu ndio mwisho wa mzozo wa kisiasa nchini." 
Wiki iliyopita, Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia alisimamisha kikao kingine cha Bunge kilichokusudia kujadili hoja hiyo ya kumuengua madarakani Spika wa bunge hilo.
Somalia imeshuhudia malumbano makali baina ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hassan Ali Khaire pamoja na kundi la wabunge wanaomuunga mkono kwa upande mmoja, na Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa upande mwingine.
Image Caption
Mgogoro huo ulianza mapema mwezi jana, baada ya wabunge zaidi ya 100 wanaoegemea upande wa Waziri Mkuu, kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kuenguliwa madarakani Spika wa bunge, kwa madai kuwa amekuwa kizingiti kwenye shughuli za bunge hilo. 
Mohamed Osman Jawari, Spika wa Bunge la Somalia anatuhumiwa na wabunge kuwa anatumia vibaya madaraka yake na kuzuia kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi hiyo. 

Sunday, April 8, 2018

RASMI ALIYEKUWA RAIS WA BRAZIL AJISALIMISHA TAYARI KUTUMUIKIA KIFUNGO

Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amewasili katika jela la Curibita kuanza kutumikia kifungo cha miaka 12 jela.
Hatua hiyo ya kujisalimisha kwa polisi ameichukua baada ya mahakama siku ya Ijumaa kumhukumu kwa mashitaka ya ufisadi. Matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vya Brazil yameonesha akiwasili kwa helikopta katika makao makuu ya polisi katika mji wa Curibita ulioko kusini mwa Brazil.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 aliondoka Sao Paoli akiwa amezingirwa na walinzi kwenye jengo la muungano wa wafuaji vyuma mjini humo. Alipenya katikati ya wafuasi wake waliokuwa wanamzuia asiondoke na kuingia katika gari la polisi. Anasisitiza kuwa mashitaka dhidi yake yalichochewa kisiasa. Lula alikutwa na hatia ya kupokea rushwa kutoka kwenye kampuni kubwa ya ujenzi, ili iweze kupata mikataba ya serikali.

UN: MYANMAR HAIPO TAYARI KUWAPOKEA WAKIMBIZI WAROHINGYA

UN: Myanmar haipo tayari kuwapokea wakimbizi Warohingya

Umoja wa Mataifa umesema Myanmar haipo tayari kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya wanaoishi kambini katika nchi jirani ya Bangladesh.

Ursula Mueller, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya siku sita nchini Myanmar na kubainisha kuwa, mazingira yalivyo hivi sasa nchini humo hayaruhusu kurejea nyumbani wakimbizi wa Rohingya.

Amesema, "Kutokokana na kile nilichokishuhudia binafsi, hali mbaya ya kiafya, ukosefu wa dhamana ya usalama na kuendelea kufurushwa kwa wakimbizi wengine kutoka mkoani Rakhine ni miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuwa Myanmar haijajiandaa kuwapokea Warohingya hao walioko Bangladesh.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya

Mwezi uliopita, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitahadharisha kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi yanayofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo, huku wakimbizi hao wakisisitiza watarejea nchini Myanmar kwa masharti mawili; mosi, wadhaminiwe usalama wao na pili wapewe uraia.

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar tangu mwezi Agosti mwaka jana katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi, yamepelekea zaidi ya Waislamu laki saba kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Thursday, April 5, 2018

JESHI LA YEMEN LASHAMBULIA TENA KWA KOMBORA SHIRIKA LA MAFUTA LA SAUDIA ARAMCO

Jeshi la Yemen lashambulia tena kwa kombora Shirika la Mafuta la Saudia Aramco
Kwa mara nyingine, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Harakati ya Kiislamu ya Answarullah, limeshambulia kwa kombora ghala la kuhifadhia mafuta la Shirika kubwa la Mafuta nchini Saudia Aramco katika mji wa Jizan, kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Yemen imesema kuwa, kombora lililotumika kushambulia ghala hilo la mafuta ni aina ya Badr-1 na kwamba lilifyatuliwa jana usiku. Wakati huo huo duru za serikali ya Saudia zimedai kwamba, ngao ya kuzuia makombora ya nchi hiyo lilifyatua kombora na kuliharibu kombora hilo la jeshi la Yemen kabla ya kufika eneo lengwa.
Kombora la Badr-1 la Answarullah
Hili ni shambulio la pili la kombora la balestiki kufanywa na jeshi la Yemen na Harakati ya Answarullah dhidi ya shirika la mafuta la Saudia katika kipindi cha wiki moja. Alkhamisi iliyopita pia, jeshi la Yemen lililishambulia kwa kombora la balestiki shirika kubwa la uzalishaji mafuta la Saudia ambapo wakati viongozi wa Riyadh wakidai pia kwamba kombora hilo lilizuiliwa, baadhi ya duru zilisema kuwa, kombora hilo lilifika eneo lengwa. Kadhalika viongozi wa Saudia walidai kwamba tarehe 25 mwezi jana, jumla ya makombora saba yalivurumishwa kutoka nchini Yemen ambapo matatu kati yake yalianguka katika mji wa Riyadh.
Hujuma za Saudia dhidi ya maeneo ya raia nchini Yemen
Mashambulizi ya makombora ya harakati ya Answarullah na jeshi la Yemen yanajiri huku hujuma za Saudia kwa kushirikiana na nchi kadhaa za Kiarabu na Magharibi dhidi ya Yemen zikiwa zimeingia mwaka wa nne. Aidha uwezo wa makombora ya harakati hiyo unashuhudiwa huku Yemen ikiwa imewekewa mzingiro wa kila upande na nchi wavamizi.

Monday, April 2, 2018

JESHI LA YEMEN LASHAMBULIA KITUO CHA JESHI LA SAUDIA ENEO LA JIZAN

Jeshi la Yemen lashambulia kituo cha Jeshi la Saudia eneo la Jizan
Jeshi la Yemen likishirikiana na wapiganaji wa Harakati ya Ansarullah wamevurumisha kombora la balisitiki ndani ya ardhi ya Saudi Arabia na kulenga kituo cha kijeshi katika eneo la Jizan.
Taarifa zinasema kombora ambalo limetumika katika oparesheni hiyo ni Qaher M-2 ambalo limetengenezwa ndani ya Yemen. Shirika la Habari la Yemen, Saba, limesema kombora hilo limesababisha hasara kubwa katika kituo hicho cha jeshi la Saudia. 
Jumamosi pia Kitengo cha Makombora cha Harakati ya Ansarullah ya Yemen kilitangaza kuwa kimevurumisha kwa mafanikio kombora la balistiki ambalo limelenga kituo cha Jeshi la Saudia katika mkoa wa Najran kusini mwa ufalme huo.
Halikadhalika Ijumaa Harakati ya Ansarullah ilitangaza kuwa ililenga kwa mafanikio kituo cha mafuta cha kampuni ya Aramco ya Saudia katika mkoa wa Jizan. Kombora lililotumika katika iparesheni hiyo pia nia Badr-1. Aidha Jumatatu liyopita wapiganaji wa Ansarullah wakishirikiana na Jeshi la Yemen walishambulia kwa makombora ya balistiki uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid katika mji wa Riyadh mji mkuu wa Saudia, uwanja wa ndege  wa Abha huko Asir na uwanja wa ndege wa Jizan unaopatikana kusini mwa Saudi Arabia. 
Watoto ni waathirika wakuu wa hujuma za Saudia dhidi ya Yemen
Mashambulizi hayo yote ni katika oparesheni za kulipiza kisasi jinai za Saudia dhidi ya raia wa Yemen. Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha hujuma yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi aliyejiuzulu urais na kukimbilia mji mkuu wa Saudia, Riyadh. 
Raia zaidi ya elfu 14  wa Yemen wameuawa, hasa wanawake na watoto, na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi. Aidha watu karibu milioni moja wameambukizwa ugonjwa wa kipindupindu kote nchini Yemen huku wengine karibu 3,000 wakifariki dunia tokea mwezi Aprili mwaka jana. Mamilioni ya Wayemen pia wamepoteza makazi yao kutokana na hujuma hizo za Saudia.